MGOGORO WA ARDHI MKURANGA WATUA KWA RAIS MAGUFULI, AAMUA KUTOA MAAGIZO MAZITO
RAIS Dk.John Magufuli ametoa maagizo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa ardhi yenye ukubwa wa hekta 1,750 unaohusisha wananchi wa kijiji cha Magodani na muwekezaji.
Kwa mujibu wa wananchi wa Mkuranga wamesema mgogoro huo ni wa muda mrefu lakini hadi sasa hakuna ufumbuzi , hivyo wametoa ombi kwa Rais Magufuli kuwasaidia kupata ufumbuzi wa eneo hilo ambalo sasa limesababisha wanyanyasike na wala kusikilizwa na viongozi wa wilaya hiyo.
Rais ametoa maagizo hilo leo Julai 30,2020 aliposimama kusalimiana wananchi hao alipokuwa akitoa mkoani Mtwara alikokwenda kwenye mazishi ya aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Mkapa ambaye amepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele jana kijijini kwake Lupaso.
Akiwa eneo hilo la Mkuranga Rais Magufuli aliomba kusikia kero za wananchi wa eneo hilo na ndipo lilipoibuka suala la mgogoro wa ardhi ambao ni wa siku nyingi kati yao na muwekezaji anayemiliki eneo la kijiji zaidi ya 1,750 ambalo amepewa kiujanja ujanja na ameshindwa kuliendeleza kwa muda mrefu.
Baada ya maelezo hayo, Rais Magufuli amesema lazima mgogoro huo upate ufumbuzi haraka."Katika nchi hii huwezi kukaa na ardhi hekta 1000 wakati hujaziendeleza, ilitakiwa ardhi iwe imefutwa zamani, hiyo ndio sheria ya nchi yetu, hauwezi ukapewa ardhi , ukaacha kuiendeleza halafu ukafanya ujanja na Halmashauri kwa kupima maeneo ya viwanda.
"Wakati ardhi haikuendelezwa, sasa nataka mfanye mchakato , wewe DC,Naibu Waziri Ulega, pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi leteni hati niifute.Mfanye mchakato niifute, ikashafutwa itagawanywa , nitaikata kati, ili inayoendelezwa iendelezwe na nyingine nitakagawa kwa wananchi bure.
"Mkuranga hoyee, huo ndio uamuzi wangu, huyo anayetaka kwenda mahakamani aende akanishataki mimi , unaweza ukaona ukweli ardhi usipoindeleza lazima ivamiwe, na ndio maana hawa watu wameingia mule wakakuta pori na ndio maana huyu jamaa akafanya ujanja na halmashauri yenu.
"Na mimi nayajua ya hapa, hata mwenyekiti wa halmashauri haelewani na dc, kwani nasema uongo ,migogoro ya kila aina iko hapa, unafikiri sijau, nataka hili liishe, na likiletwa kwangu nitafuta, na mlete na mapendekezo, kama yulu mwekezaji anatosha kuwekeza apewa.
"Linalobaki lingine wapewe wananchi bure wala sio kwa kuliuza, mlioleta mgogoro ni halmashauri kwasababu mlizungumza naye ukaingia ujanja ujanja mkisema mnapima na ardhi, mbona hakuna kiwanda kilichojengwa huku, kwa hiyo DC makero haya hayatakiwi kuja kwa mtu niliyemteua,"amesema Rais Magufuli.
Amemwambia DC kwamba anafahamu anafanya kazi nzuri lakini kwenye mgogoro huo hapana huku akieleza anafahamu aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Abdalla Ulega anafanya kazi zake vizuri na kumataka ashughulikie mgogoro huo.
"Kazi ya Naibu Waziri, Waziri na Mbunge ni kushughulikia matatizo ya watu, hayawezi kuwa yananisubiri mimi mpaka nifike hapa ndio muanze kushughulikia, mimi ni mmoja tu na mimi ni binadamu , kwa hiyo hili litafutiwe ufumbuzi, akitaka aende mahakamani hata mara 10, mmenielewa?"alihoji Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais kabla ya kutoa maagizo hayo alisikiliza wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga pamoja na Mbunge wa jimbo la Mkuranga Ulega ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi na kisha kutoa maelekezo ya suala hilo kutafutiwa ufumbuzi na yuko tayari kulifuta kwani yeye ndio msimamizi wa ardhi yote nchini.
No comments: