TAKUKURU MANYARA YAMSHIKILIA ALUTE KWA MIKOPO UMIZA
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, inamshikilia mkazi wa Mjini Babati, Japhet Samwel Alute kwa kudaiwa kufanya biashara ya mikopo umiza inayoambatana na kukopesha wananchi kwa riba kubwa na kisha kuwadhulumu mali zao wanazoweka kama dhamana.
Mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza jana mjini Babati alisema Alute anafanya bishara hiyo bila kuwa na leseni ya biashara jambo ambalo linaikosesha Serikali mapato kutokana na ukwepaji wa kodi.
Makungu alisema biashara ya fedha inatakiwa kupata kibali cha Benki Kuu ya Tanzania, jambo ambalo Alute hajalitekeleza na pia hana leseni ya kufanya biashara.
Alisema Alute pia anatumia jina la Halmashauri ya Mji wa Babati, kuwatishia wananchi wanaochelewa kufanya mrejesho kwa kuwatumia ujumbe wa kuuza maeneo yao au nyumba walizoweka dhamana kwa mikopo umiza.
``Alute alipekuliwa na kukutwa akiwa na mikataba ya kitapeli 99 ambayo inaonyesha ameuziwa maeneo mbalimbali zikiwemo nyumba na viwanja vya wananchi wa hapa mjini Babati,`` alisema Makungu.
Alisema Alute pia alikutwa na vitambulisho vya watumishi wa umma na vitambulisho vya uraia wa Tanzania ambavyo siyo mali yake.
``Tunatoa wito kwa wana Manyara wote ambao kwa namna moja au nyingine wamekumbana na mikopo umiza ya Alute au mali zao kuchukuliwa kutokana na mikopo umiza hiyo wafike ofisi za Takukuru,`` alisema Makungu.
Alisema wahusika hao wafike ofisini kwao mjini Babati, jumatatu ya Agosti 3 mwaka huu ili changamoto ya mikopo umiza ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Babati.
No comments: