WAKAZI WA KIGOMA WAITIKIA WITO KUTOA DAMU SALAMA KWA HIYARI


Na Editha Karlo-Michuzi TV

MENEJA  wa mradi wa damu salama mkoa Kigoma, Habichi Maramba amesema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi wa mkoa Kigoma kujitokeza kutoa damu kwa hiari jambo ambalo linaondoa changamoto ya ukosefu wa damu mkoani humo.

Maramba alisema hayo wakati wa maadhimisho ya wiki ya damu salama mkoani Kigoma na kueleza kuwa  jambo hilo linaenda sambamba na uundwaji wa vikundi vya wachangia damu mkoani humo ambavyo vimesaidia kupatikana kwa damu ya kutosha.

Meneja huyo wa damu salama mkoa Kigoma alisema kuwa hadi sasa jumla ya vikundi 46 vimeundwa vikiwemo vikundi vya waendesha bodaboda na makundi mbalimbali ya kijamii ambavyo damu inayopatikana imesaidia kituo cha damu salama kuwa na damu ya kutosha wakati wote.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa Kigoma, Oseah William alisema kuwa ongezeko kubwa la ajali zitokanazo na pikipiki maarufu boda boda limechangia onezeko kubwa la mahitaji ya damu mkoani Kigoma.

William alisema kuwa  pamoja na ongezeko la ajali za boda boda na ongezeko la mahitaji ya damu mkoa umejipanga kuhakikisha hakuna tatizo la upatikanaji wa damu hali inayofanya kuendeshwa kwa mpango wa ukusanyaji wa damu salama ili kuhakikisha benki ya damu inakuwa na damu ya kutosha  wakati wote.

Sambamba na hilo alisema kuwa ongezeko la vituo vya afya vinavyofanya upasuaji na kuongeza damu kukiwa na vituo 13 ambavyo vimechangia kuongeza mahitaji ya damu mkoani humo huku mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua ni eneo linalopewa kipaumbele kuhakikisha tatizo la damu haliathiri kundi hilo.

 Baadhi ya wananchi waliojitokeza kutoa damu kwa hiari katika maadhimisho hayo akiwemo Siwema Masudi mkazi wa Kibirizi Manispaa ya Kioma Ujiji alisema kuwa wamehamasika kujitokeza kutoa damu kwa hiari ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji damu na hasa wale wa dharula. 
 Meneja wa mradi wa damu salama mkoa Kigoma Habichi Maramba akiongoza wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji kutoa damu katika maadhimisho ya wiki ya damu salama ambayo kimkoa yalifanyika mjini Kigoma kwenye viwanja vya ofisi za redcross.
 Mwandishi wa habari wa ITV mkoani Kigoma Kassim Msoma akitoa damu kwa hiari katika maadhimisho ya damu salama yanayosimamia na mradi wa damu salama unaoendeshwa na Tanzania Red Cross Society
 Wakazi wa manispaa ya kigoma Ujiji waliojitokeza kutoa damu kwa hiari wakati wa maadhimisho ya damu salama ambayo yalifanyika kimkoa kwenye manispaa ya Kigoma Ujiji.
 

No comments: