JOTO LA URAIS CHADEMA LAPAMBA MOTO, MCH MSIGWA ATAJA MAMBO MATATU ATAKAYOYAFANYA AKIWA RAIS
Charles James, Michuzi TV
UCHUMI imara, kusimamia utawala bora na kuboresha elimu nchini, ndivyo vipaumbele vitatu ambavyo Mtia nia wa Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mch Peter Msigwa amevitaja.
Mch Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini ametangaza rasmi nia yake hiyo ya kugombea Urais kupitia Chadema leo jijini Dodoma ambapo pia alisindikizwa na wabunge wenzake, Godbless Lema, Joseph Mbilinyi 'Sugu' Hawa Mwaifunga na John Heche.
Akizungumza na wandishi wa habari wakati wa kutangaza nia yake hiyo, Mch Msigwa amesema endapo atapata ridhaa ya kuwa Rais atahakikisha anafumua muundo mzima wa Elimu nchini na kuweka mwingine utakaokua na matokeo chanya kwa Taifa.
Amesema mfumo wa elimu uliopo hivi sasa unaegemea zaidi vyeti na wala hauwapi wasomi mwanga wa kuwa wataalamu wa kuvumbua zaidi badala yake wanakua tegemezi ilihali ni wasomi.
" Nikipata ridhaa ya kuwa Rais nitahakikisha nafanya maboresho makubwa kwenye elimu, ni lazima tuwe na Nchi ya wavumbuzi wanaotafuta suluhihisho kitaalamu, tuondokane na elimu ya vyeti ambayo kwa miaka 50 imeshindwa kuwakomboa watanzania.
Kama Taifa hatuwezi kufanikiwa kwa kuwa na watu wenye fikra ndogo, tofauti yetu na wenzetu walioendelea ni upanuzi wa fikra na ukubwa wa elimu yao, tunapaswa kuwekeza kwenye elimu kama kweli tunataka kufikia uchumi wa kati unaotokana na viwanda, " Amesema Mch Msigwa.
Akizungumzia ukuaji wa uchumi, Mch Msigwa amesema mfumo uliopo pia unahitaji mabadiliko makubwa kwani huu wa sasa umepitwa na wakati na hauwezi kuwasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
Amewaomba watanzania watakapoenda kuchagua Rais Oktoba 25 mwaka huu wachague Kiongozi mwenye maono ya kuwavusha kiuchumi na mwenye uwezo wa kuvutia wawekezaji na kutoa wigo mpana pia wa watanzania wenye kujiajiri.
" Suala la utawala bora nitalisamamia kwa kuhakikisha pia tunarudish mchakato wa katiba mpya ambao utawezesha kubadilisha sheria kandamizi ambazo zimekua hazina msaada kwa watanzania zaidi ya kuwakandamiza.
Kupitia mchakato wa katiba mpya naamini pia tutapata tume huru ya Uchaguzi ambayo itamaliza kiu ya watanzania lakini pia kuweka mgawanyo wa kimadaraka," Amesema Mch Msigwa.
Mch Msigwa anakua mwanachama wa tatu wa Chadema kutangaza nia ya kugombea Urais hadharani baada ya wanachama wawili Mayjose Majinge na Makamu Mwenyekiti wa Chadema hiko, Tundu Lissu kutangaza azma yao ya kugombea kupitia chama hiko kikuu cha upinzani.
Mtia nia wa Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, Mch Peter Msigwa akizungumza na Viongozi waliojitokeza kumsikiliza, Wanachama wa Chadema na Wandishi wa habari jijini Dodoma leo.
Mtia nia wa Urais kupitia Chadema, Mch Peter Msigwa akizungumza na wandishi wa habari leo wakati akitangaza rasmi lengo lake la kuwania Urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wabunge John Heche wa Jimbo la Tarime Vijijini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' wakiwa na wanachama wengine wa Chadema wakifuatilia mkutano wa Mch Msigwa wa kutangaza nia ya kugombea Urais kupitia chama hiko leo jijini Dodoma.
No comments: