MZABUNI WA MADIRISHA UJENZI WA IKULU NDOGO HANANG AKAMATAWA NA TAKUKURU

Charles James, Michuzi TV

BAADA ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Hanang Mkoani Manyara kubaini madirisha yaliyowekwa katika ujenzi wa Ikulu Ndogo unaoendelea wilayani hapo hapo chini ya kiwango umemkamata na kumshikilia Joakimu Kauki kwa tuhuma hizo.

Kauki ndiye aliyepewa tenda ya uzabuni ya kutengeneza madirisha ya Aluminum na ofisi ya manunuzi Mkoa wa Manyara kwa jengo la Ikulu Ndogo inayojengwa wilayani Hanang.

Uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU umebaini pia Mzabuni huyo alipewa kandarasi hiyo na idara ya manunuzi Mkoa kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma.

Kwa mujibu wa BOQ Mzabuni alitakiwa kutengeneza na kuweka kwenye jengo hilo madirisha ya Aluminium yenye kioo cha unene ya 6mm lakini badala yake Mzabuni akatengeneza na akapeleka eneo la ujenzi madirisha yenye kioo cha unene wa 5mm.

Katika ufuatiliaji wa mradi huo ikiwa ni Moja ya majukumu ya TAKUKURU walibaini dirisha hizo ziko chini ya kiwango kilichoainishwa kwenye BOQ.

" Baada ya kubaini hilo TAKUKURU wilaya ya Hanang walichukua hatua za kumuagiza Mzabuni asiyatumie madirisha hayo kwenye jengo hilo hadi atakapoleta madirisha yenye kiwango kilichoainishwa katika BOQ na kufanyiwa ukaguzi ili kujiridhisha na ubora kama ambavyo wamefanya kwenye miradi mingine.

Kufuatia zuio letu hilo Mzabuni alimweleza Mhandisi wa Mkoa Eng Dominicianus Kilina kwa njia ya simu ambaye bila hata ya kuwasiliana na Takukuru alielekeza madirisha hayo yafitishwe yakiwa hivyo hivyo," Amesema Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Manyara.

Baada ya TAKUKURU kupata taarifa hiyo ya kudharau maelekezo yao walielekeza mzabuni na mafundi wote kukamatwa kwa uchunguzi wakati mhandisi Kilina akitafutwa kusaidia uchunguzi huo.

No comments: