UHARIBIFU WA MAZINGIRA KUKABILIWA NA MKAA MBADALA

Mbunifu wa mashine ya mkaa utokanao na vumbi la mbao pamoja na pumba za mpunga wa mkoani Singida, Joram Kishaluli akitoa mkaa uliotengenezwa kwa mashine maalumu.

Na, COSTECH
TAARIFA ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2019 inaonesha kuwa, kwa miaka mitano iliyopita kuanzia msimu wa mwaka 2013/2014 hadi 2017/18, Tanzania imezalisha chakula kingi kuliko mahitaji yake.


Tathmini ililenga hali ya chakula, uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wa chakula hususani mazao muhimu yanayozingatiwa kama mahindi, mtama, ulezi, mchele, mikunde, ngano, ndizi, mihogo na viazi.


Katika kipindi hicho, Tanzania imejitosheleza kwa kati ya asilimia 120 hadi 125 na kuzalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,322,689.


Tathmini kuhusu uzalishaji ilifanywa na Wizara ya Kilimo kati ya Mei hadi Juni 2019 kwa msimu wa 2018/2019 na nyingine kuhusu upatikanaji wa chakula ilifanywa kwa mwaka 2019/2020 zilionesha uzalishaji wa mazao ya chakula utafika tani 16,408,309 zikiwamo tani 9,007,909 za nafaka na tani 7,400,400 za mazao mengine. 


Makadirio hayo ni sawa na kupungua kwa tani 483,665, ambapo nafaka hasa mahindi yalishuka kwa tani 455,642 na mchele tani 210,44 wakati mazao yasiyo ya nafaka yakiongezeka kwa tani 46,283.

Kwa msimu wa 2018/2019 mchango wa mahindi ulikuwa asilimia 35, muhogo kwa asilimia 17, mchele kwa asilimia 12, viazi kwa asilimia 10 na mazao mengine.
Mkaa Mbadala ukiwashwa 

Pamoja na mwenendo huo mzuri wa uzalishaji na usalama wa chakula, kuna changamoto kadhaa zilizopo katika jamii, nazo ni uharibifu wa mazingira unaotishia kilimo pamoja na upotevu wa chakula baada ya mavuno.

Takwimu zinaonesha kuwa, chakula kingi hupotea baada ya kuvunwa huku mazao mengi yakiwa hayatumiki kwa ufasaha. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) zinaonesha kuwa, mpaka asilimia 40 za nafaka hupotea nchini baada ya mavuno.

Joram Clement Kishaluli ni mbunifu wa mashine ya mkaa utokanao na vumbi la mbao pamoja na pumba za mpunga mkoani Singida. Mradi wake upo Misuna, Singada mjini na bidhaa anazozalisha huziuza kwa wachoma chipsi na watumiaji wengine.

Akiona jitihada za Serikali na dunia nzima inavyozuia ukataji miti na kuhamasisha matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati, anasema aliumiza kichwa kuona ni kwa namna gani anaweza kuisaidia jamii kupata suluhu ya kudumu.

“Lengo la ubunifu huu ni kukabiliana na uharibifu wa mazingira hasa unaotokana na uchomaji mkaa na ukataji kuni kwa kuwapa wananchi chanzo mbadala cha nishati,” anasema Kishaluli.

Wakati anaendelea kufikiria ni kwa namna gani atasaidia kuleta suluhu ya matumizi ya kuni na mkaa yanayochangia uvunaji holela wa misitu, anasema siku moja alimtembelea rafiki yake mwenye mashine ya kukoboa mpunga na kukuta kuna lundo kubwa la pumba.

“Nilimuuliza anazifanyia nini akaniambia huwa anazichoma ingawa mamlaka hazitaki afanye hivyo kwani anachafua mazingira. Basi nikamwambia tutengeneze mkaa ndipo mkakati mzima ulipoanzia,” anasema mbunifu huyo.

Kabla ya mkaa, kwanza anasema alianza kutengeneza mashine ya kutengeneza mkaa huo mwaka 2014 ambayo ilikamilika mwaka 2019 na akapata oda ya tani 30 jijini Dar es Salaam kutokana na faida ya mashine hiyo kutokutoa moshi.

“Mteja wa Dar es Salaam alikuja akaomba sampuli, tulimpa kilo 20 na aliporidhika ndipo akatoa oda ya tani 30,” anasema.

Kilo moja ya mkaa huo anasema wanaiuza Sh600 na jiko lake Sh90,000. Mkaa unaweza kuwashwa halafu ukazimwa kama mhusika amemaliza kupika kisha ukawashwa baadaye.

COSTECH
Kukua kwa soko lake anasema kwa namna au nyingine kumechangiwa na ushiriki wake kwenye Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (Makisatu) yanayoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi an Teknolojia (COSTECH).


Kabla hajaorodheshwa kushiriki mashindano hayo, anasema alipokea dodoso la Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) lililolenga kuwatambua na kuwasajili wabunifu, hivyo akasajili ubunifu wake uliokubalika na akakutanishwa na COSTECH.

Baada ya dodoso la Sido, wataalamu wa Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi (Veta) walimfuata.

“Taasisi hizi mbili ndizo zimenifanya Serikali initambue. Mwaka jana nilibahatika kushiriki Makisatu na kuhudhuria maonesho kadhaa yaliyonikutanisha na wadau wengi wengine hivyo kutanua soko langu,” anasema.

Kutokana na ushiriki wake kwenye Makisatu, anasema mwaka jana ametembelewa na watu wengi sana waliotaka kuuona mradi wake.

Hao wote, anasema, walikuwa na mawazo mazuri waliyoyatoa baada ya kuzungumza nao hivyo hakuna haja ya mbunifu kujificha.

Ushauri
Endapo Serikali itaendeleza kasi hii ya kuwajali wabunifu, anasema anaiona Tanzania itafika mbali katika utatuzi wa changamoto zilizopo katika jamii.

Kabla ya kupata ruzuku ya COSTECH, anasema alikuwa anatumia fedha zake za mfukoni lakini Costech imemsaidia kununua mtambo wa kutengeneza majiko yanayotumia mkaa huo mbadala.

“Naamini nitaanza kutengeneza majiko ya kutosha na kuyasambaza nchi nzima ili yatumike kukabili sababu za kutumia mkaa na kuni vinavyochangia uharibifu wa mazingira, anasema.Kutokana na changamoto zilizopo anashauri Serikali iangalie uwezekano wa kuwa na karakana ya umma itakayotoa fursa kwa wabunifu mbalimbali kuitumia.

Miaka ya nyuma anakumbuka kulikuwa na kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools ambacho kilikuwa muhimu kwa upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika na wabunifu.

No comments: