WAFANYABIASHARA VIFAA VYA UMEME DAR WALALAMIKIA NYAYA ZISIZO NA UBORA,WAIOMBA TBS KUFANYA MSAKO
BAADHI ya wafanyabiashara ya kuuza vifaa vya umeme vya aina mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam wamelalamikia uwepo wa vifaa hivyo na hasa nyaya ambazo ziko chini ya kiwango na ubora ambazo zinatengenezwa na baadhi ya viwanda vilivyopo nchini, hivyo wametoa ombi kwa Serikali kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na tume ya ushindani (FCC) kufanya msako viwandani na madukani ili kubaini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika maeneo ya Kariakoo jijini Dar es Salaam, baadhi ya wafanyabiashara hao pamoja na wanunuzi wa bidhaa hizo wamedai kumekuwepo na wimbi kubwa la uzalishaji wa bidhaa hizo hasa nyaya za umeme za majumbani ‘wiring’ zisizo na viwango unaohitajika.
Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme Rashid Salum pamoja na Frank Mtonga waliopo eneo hilo la Kariakoo wamesema kwamba uwepo wa bidhaa hizo zilizo chini ya ubora umesababisha maduka yanayouza bidhaa zenye viwango bora kukosa wateja kutokana na wananchi wengi kukimbia kwa kigezo cha bei na kuzifuata nyaya zisizo na ubora kutokana na unafuu wa bei bila kujua athari zake.
Kwa upande wake Salum amesema kuna maduka mengi hasa maeneo ya mitaa ya Narung'ombe na maeneo mengine yanye maduka yanayouza bidhaa hiyo huku akifafanua wapo wanauza nyaya ambazo hata ukizitamaza kwa macho utabaini hazina ubora na kigezo kikubwa kinachofanya wananchi wazikimbile ni unafuu wa bei” alisema Salum
Bila kutaja majina ya viwanda vinavyotengeneza nyaya hizo, Salum amesema kimsingi nyaya hizo pamoja na baadhi ya vifaa vingine vya umeme, vinazalishwa kutoka katika viwanda vinavyomilikiwa na raia wa kigeni wasio waaminifu na kuiomba Serikali kufuatilia kwa undani ili kubaini.
Wakati Mtonga amesema yeye kama mfanyabiashara aliwahi kupokea lawama kutoka kwa baadhi ya wateja wake, waliomtuhumu kuwauzia nyaya zisizo na ubora, suala alilodai kuwa hakulifahamu kwa kuwa hakuwa na uelewa wa kutosha juu ya nyaya hizo na viwango vyake.
Hivyo ameiomba TBS kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka pamoja na viwandani hatua itakayosaidia kuwabaini wahusika kisha kuchukuliwa hatua kulingana na sheria na taratibu za nchi kwa madai kuwa wengi wa wenye viwanda hivyo wamekuwa wakifanya hayo kwa makusudi licha ya kujua athari za kufanya hivyo.
Ametoa mfano kuwa kwa nyaya zenye ubora wa viwango ambazo zinauzwa kwa wastani wa Sh 100,000, huuzwa kwa wastani wa hadi 70,000 kwa nyaya zisizokuwa na ubora wa viwango na hivyo kuathiri ushindani wa bei katika sokoo huku pia zikileta madhara kwa wananchi yakiwemo ya nyumba kuungua.
"Tunawaomba TBS pamoja FCC kuendesha ukaguzi wao wa mara kwa mara katika maduka yanaouza bidhaa za umeme lakini pamoja huko kwenye viwanda zinapozalishwa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua wahusika kama njia moja wapo ya kukomesha biashara hiyo,"amesema.
Kwa nyakati tofauti Serikali kupitia Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani imekuwa ikisisitiza utumiaji wa vifaa vya umeme vyenye ubora vinavyozalishwa hapa nchini na kupiga marufuku uzalishaji wa vifaa vyote visivyo na ubora, agizo linaloonekana kupuuziwa na baadhi ya wenye viwanda hivyo.
No comments: