NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII KANYASU AKERWA NA WAVAMIZI WA MAENEO YA HIFADHI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akioneshwa eneo na Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, Felix Mwasenga katika Ushoroba wa Kwakuchinja ambao ni muhimu kwa mapito ya wanyamapori wanaotoka katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuelekea HIfadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara ukiwa umevamiwa na baadhi ya wananchi wanaoendesha shughuli za kibinadamu katika wilaya ya Babati mkoani Manyara. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Babati, Mhe, Elizabeth Kitundu

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Chem chem, Nicolaus Negri ambaye ni Mwekezaji katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge ( WMA) mara baada ya kuwasili katika Hoteli ya Chemchem iliyopo ndani ya Jumuiya hiyo ya Burunge katika wilaya ya Babati mkoani Manyara

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa na Mkurugenzi wa Chem chem, Nicolaus Negri pamoja na kamati ya Ulinzi na usalam ya wilaya ya Babati wakitembelea kujionea wanayamapori mbalimbali katika eneo la Mwekezaji huyo aliyekeza Hoteli ya Kitalii katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akipewa zawadi kabla ya kuagana na Mkurugenzi wa Chem chem, Nicolaus Negri wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya ya kutembelea Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge iliyopo katika wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akiwa kwenye picha ya pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya ya Babati katika Hoteli ya Chem Chemi iliyopo ndani ya Jumuioya ya Hifadhi ya Burunge inayounganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Jumuiya ya HifAdhi ya Wanyamapori ya Burunge iliyopo katika wilaya ya Babati mkoani Manyara,
…………………………………………………………………………….
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameonesha kukerwa na baadhi ya wananchi wanaendelea kujenga nyumba na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo yenye Wanyamapori hasa katika mapito ya Wanyamapori katika eneo la Kwakunchinja linalounganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Manyara. 

Amesema kutokana na tabia hiyo Serikali haiwezi kumaliza kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa wananchi wanaoshambuliwa na wanyamapori wakali na waharibifu

Ameyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA) iliyopo wilaya ya Babati mkoani Manyara kuona namna ya kulinda ushoroba wa Kwakunchinja ambao ni umuhimu kwa Wanyamapori wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuelekea Hifadhi ya Ziwa Manyara.

Amesema kwa mwaka huu pekee Serikali imetumia kiasi cha shilingi Bilioni moja kulipa vifuta jasho na vifuta machozi huku kiasi cha shilingi Bilioni 2.3 ikiwa bado hakijalipwa kwa wananchi walioathiriwa na Wanyamapori wakali na Waharibifu  Amesema kila mahali wananchi wamekuwa wakilalamikA kuchelewa kulipwa vifuta jasho na vifuta machozi kutokana na madai hayo kuwa mengi hali inayopelekea Wizara kuwa na madai mengi yasiyolipika kutoka kwa wananchi ambao baadhi wameyafuata makazi ya Wanyamapori

Hata hivyo, Mhe.Kanyasu amesema Serikali inatafuta mbinu mbadala ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu baada ya kugundua kuwa fidia sio suluhisho kutokana na wimbi kubwa la wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu katika shoroba za wanyamapori pamoja na maeneo ya mitawanyiko ya wanyamapori . 

Amesema kutokana na tabia ya baadhi ya wananchi kufanya makazi katika maeneo hayo, Wizara ya Maliasili na Utalii imegundua hata ikitenga bajeti nzima ya Wizara kwa ajili ya kulipa vifuta jasho na vifuta machozi haitaweza kumaliza tatizo hilo. Mhe.Kanyasu amesema binadamu wamekuwa wakiwafuata Wanyamapori hivyo suala la mazao ya kushambuliwa ni jambo lisiloepukika .

“”Sehemu ya Mapori ya Akiba na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori ndimo Wananchi wameanzisha makazi hivi unategemea wanyamapori watulie tu ” alihoji Kanyasu. Amefafanua kuwa Wananchi waliojenga katika maeneo hayo wamekuwa wakitoa visingizio kuwa ardhi imepungua na hivyo kuwalazimu kuanzisha shughuli za binadamu katika maeneo ya wanyamapori suala ambalo ni umekuwa ni mzigo kwa Serikali ya kuanza kulipa fidia kila mwaka. 

Amesisitiza kuwa shida sio ardhi bali wananchi wameshindwa kutumia ardhi waliyonayo kimipango hata hivyo Wananchi walio wengi wanataka kufuga mifugo kwa idadi kubwa na sio kwa ubora. 

Pia, Akizungumzia Kilimo, Mhe.Kanyasu amesema Wakulima wamekuwa wakilima kizamani kwa kuamini kulima eneo kubwa ndio kupata mazao mengi jambo ambalo si kweli. Amesema shida kubwa inayoikabili nchi kwa sasa ni ongezeko kubwa la binadamu na mifugo ilhali ardhi haiongezeki. 

Amesema hali hivyo imechangia maeneo ya Hifadhi kuvamiwa kwa ajili ya kilimo na makazi kwa vile maeneo hayo yamehifadhiwa na hiyo haimaanishi kuwa hakuna vijiji vyenye maeneo kwa ajili ya makazi na malisho ya mifugo. 

” Vijiji vyote vina mabonde, vijiji vyote vina maeneo ya malisho lakini yameharibiwa kutokana na idadi kubwa ya mifugo na mengine yameharibika kwa vile hayatunzwi” alisisitiza Kanyasu
Kufuatia hali hiyo, Mhe.Kanyasu amezitaka taasisi za Uhifadhi nchini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua umuhimu wa maeneo yaliyohifadhiwa la sivyo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori haitaisha. 

Hata hivyo, Amewataka wananchi kubadili mfumo wa maisha kwa kuacha kufuga kimazoea badala yake wafuge kisasa na pia waachane na kilimo cha kuhama hama ambacho kutokana na ongezeko la idadi ya watu hakifai kwa sasa .

No comments: