NI WAJIBU WA MFANYABIASHARA WA VYUMA CHAKAVU KUFUATA SHERIA-SIMA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mussa Sima akizungumza na wafanyabiashara wa vyuma chakavu kutoka badhi ya mikoa (hawapo pichani) jijini Tanga. Wengine pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martine Shigela na Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mhe. Thobias Mwilapwa.

…………………………………………………………………………..

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) amesema ni wajibu wa kila mfanyabiashara wa vyuma chakavu kufuata sheria ili kulinda miundombinu na kuepuka migogoro.

Sima ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wafanyabiashara hao katika mkutano uliofanyika jijini Tanga na kuwataka kuwa na vibali vya biashara hiyo.

Pamoja na mambo mengine naibu waziri huyo alisema Serikali haitawatoza faini kwa mizigo ya vyuma chakavu walizohifadhi na badala yake watatakiwa kuomba vibali upya ili waendelee kufanya biashara.

“Ndugu zangu hapa tunazumgumzia ule mzigo ulio nao na sio ule utakaokuwa nao baadae maana kuna wengine watafikiri tumesema kuwa hata baadae ukiwa nao mzigo hautachajiwa faini, hapana kuanzia sasa kwenye kikao hiki mtu mwenye mzigo atuambie tufahamu,” alisisitiza.

Alisema jukumu la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mtu anafuata sheria zilizowekwa huku akitoa rai kwa wafanyabiashara hao kuunda ushirika wa idadi ya watu waliokubaliana kwa pamoja na suala la vibali litakuwa jambo rahisi kwao.

Aidha Sima alisema Serikali inafanya kazi kwa ukaribu na wafanyabiashara hao lakini nao wanapaswa kutii maelekezo na kufuata sheria zilizowekwa ili kuepuka migogoro isiyo na ulazima.

“Mwaka 2019 tulitengeneza kanuni hivyo kila mmoja wetu analazimika kuwa na kibali na sisi tunawajibika kutoa kibali na kama kuna changamoto ya utoaji wa vibali hivi tunajadili kwa pamoja wapi tuna tatizo na tunatatua na pia hatuko hapa kuizuia biashara hii,” alisema.

Kwa upande wao wafanyabiashara hao wakiwasilisha malalamiko yao walidai kutozwa kiasi cha sh. milioni 1.5 kwa mwaka wakidai ni kikubwa tofauti na mitaji yao.

Waliongeza kwa kuahidi kuwa wao kama wananchi watatekeleza maelekezo ya Serikali ya kuyafanya biashara hiyo kwa kulipia vibali vinavyohitaji bila bugudha yoyote.

Waliahidi kufuata sheria na kuwa jumuiya ya wafanyabiashara watakuwa mabalozi kwa wenzao kuhakikisha wanalipia vibali husika kwani vibali vinapokuwa rafiki hakuna haja ya kufanya biashara bila kufuata sheria.

No comments: