RADIO FARAJA YAKABIDHI MSAADA KWA KAYA ZENYE KIPATO CHA CHINI KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA




Na Simeo Makoba - Shinyanga.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ng’habi amekabidhi msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo vyakula na fedha taslimu kwa wazee wasiojiweza ambayo imechangwa na wadau mbalimbali wa Radio Faraja Fm Stereo iliyopo Mjini Shinyanga.

Ng'habi aliyekuwa ameongozana na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa serikali za mitaa Manispaa ya Shinyanga Nassor Warioba na Wafanyakazi wa Radio Faraja Fm Stereo amekabidhi msaada huo Jumamosi Mei 16,2020.

Baadhi ya misaada iliyotolewa kwa wazee hao ambao ni Bi. Kwangu Lugeg’ha mwenye umri wa miaka 69 mkazi wa mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyangana Mzee Furaha Lukeyemba mwenye umri wa miaka 100 ambaye pia ni mkazi wa kata hiyo ni pamoja na unga wa ngano,mchele,maharage, sabuni na fedha taslimu kiasi cha shilingi laki mbili.

Aidha kiasi cha shilingi elfu sitini kati ya fedha hizo kitatumika kuwakatia wazee hao Bima ya Afya ya Jamii Iliyoboreshwa (CHF) kwa ajili ya kuwarahisishia kupata huduma za matibabu.

Akikabidhi misaada hiyo, Ng’habi ameipongeza Radio Faraja fm Stereo kupitia kipindi cha Mambo leo kwa kufanya kampeni hiyo iliyopewa jina la “MAMBO LEO FARAJA TIME 2020” ya kuwasaidia watu wasiojiweza kwenye baadhi ya kaya wanazoishi na kubainisha kuwa, vitu vilivyotolewa vitawasaidia wazee hao kupunguza hali ya ukali wa maisha na kuomba mashirika, taasisi na watu wengine kuendelea kutoa misaada kwa wahitaji.

“Ninaomba zoezi hili lichukuliwe kama mfano kwa watu wengine kwani ukiangalia sasa hivi tumekuwa na harakati za kupunguza omba omba maeneo ya mjini, sasa kupitia njia hii itasaidia kupunguza watu wanao omba misaada mitaani na kusaidiwa kupitia familia zao”,amesema.

Bi.Kwangu Lugeg’ha mwenye umri wa miaka 69 mkazi wa mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga na Mzee Furaha Lukeyemba mwenye umri wa miaka 100 ambaye pia ni mkazi wa kata hiyo kwa pamoja wameishukuru Radio Faraja fm strereo pamoja na wote walioshiriki kuchanga ili wao kupata msaada na kusema kuwa msaada walioupata utawasaidia kwa kiasi kikubwa.

Akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Radio Faraja Fm Stereo ,Meneja Vipindi Msaidizi wa Radio Faraja Bw. Simeo Makoba ,amesema lengo la kuwashirikisha wadau kusaidia watu wasiojiweza ni kuijengea jamii moyo wa kujitoa kwa ajili ya watu wenye mahitaji walioko katika maeneo yao.

“Tumeona watu wengi wamekuwa wakitoa misaada wakielekeza kwenye taasisi zinazolea watoto yatima na wazee lakini wakati huo huo wanawaacha watu wanaoishi nao katika maeneo yao, ambao wana uhitaji lakini sisi tumeamua kufika kwenye familia zenye kuhitaji msaada wakiwemo wazee na kuwapa kile tulichojaaliwa”,amesema Makoba.

Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau waliochangia misaada hiyo ikiwemo Ofisi ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,Shirika la Umeme Tanzania TANESCO mkoa wa Shinyanga, watuma salaamu pamoja na wadau wengine kwa kuonyesha moyo wa kuguswa na matatizo ya wengine.

Hata hivyo Wenyeviti wa Mtaa wa Sanjo na Chamaguha Elias Ramadhani Masumbuko pamoja na Hussein Ramadhani wameipongeza Radio Faraja fm kupitia Kipindi cha Mambo leo kwa kufanya Kampeni ya kuwasaidia wasiojiweza na wameomba kampeni hiyo iwe endelevu kwa kuwa wenye mahitaji bado ni wengi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa wenyeviti wa serikali za mtaa Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Miti mirefu Bw. Nassor Warioba amewashauri wadau wengine ndani na nje ya Manispaa ya Shinyanga kujitokeza kwa jamii yenye uhitaji kupitia wenyeviti wa serikali za mitaa kwa kuwa wao ndiyo wanafahamu kina nani wana uhitaji katika mitaa yao.
Kushoto ni Afisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ng’habi akikabidhi pesa kwa Bibi Kwangu Lugeg’ha mwenye umri wa miaka 69 mkazi wa mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga.Fedha hizo ni sehemu ya vitu mbalimbali vilivyochangwa na wadau mbalimbali wa Radio Faraja Fm Stereo iliyopo Mjini Shinyanga. Picha zote na Samir Salum na Josephine Charles.

Afisa ustawi wa jamii wa manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ng’habi akikabidhi pesa kwa Mzee Furaha Lukeyemba mwenye umri wa miaka 100 ambaye pia ni mkazi wa kata ya Chamaguha.

Bibi Kwangu Lugeg’ha akikabidhiwa Mfuko wa Unga wa Ngano,Maharage,Sabuni na mchele.

Kushoto ni Meneja Vipindi Msaidizi wa Radio Faraja Bw. Simeo Makoba akimweleza jambo Bi. Kwangu
Kutoka Kushoto ni Meneja Vipindi Msaidizi wa Radio Faraja fm Simeo Makoba,Mwandishi wa Habari na Mtangazaji wa Radio Faraja Josephine Charles,Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga Bw.Emanuel Ng'habi,Mwenyekiti wa wenyeviti Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Miti Mirefu Nassor Warioba,Bi.Kwangu Lugeg’ha pamoja na wajukuu zake na Mwenyekiti wa mtaa wa Sanjo Bw. Elias Ramadhani Masumbuko wakipiga picha ya kumbukumbu.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa serikali za mtaa Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Miti mirefu bwana Nassor Warioba akimsaidia Mzee Furaha Lukeyemba kuhesabu pesa.

Mzee Furaha Lukeyemba akihesabu pesa baada ya kuzipokea.

Mwandishi & Mtangazaji wa Radio Faraja wa kipindi cha Mambo leo bi. Josephine Charles ambaye ndiyo mmoja wa walioanzisha Kampeni ya "MAMBO LEO FARAJA TIME 2020" akimfanyia mahojiano Mzee Furaha Lukeyemba.

Mwandishi & Mtangazaji wa Radio Faraja wa kipindi cha Mambo leo bi. Josephine Charles ambaye ni mmoja wa walioanzisha Kampeni ya "MAMBO LEO FARAJA TIME 2020" akimfanyia mahojiano Afisa Ustwi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga Bw. Emanuel Ng'habi.
Mwandishi & Mtangazaji wa Radio Faraja wa kipindi cha Mambo leo bi. Josephine Charles ambaye ni mmoja wa walioanzisha Kampeni ya "MAMBO LEO FARAJA TIME 2020" akimfanyia mahojiano Meneja vipindi msaidizi wa Radio FARAJA Bw. Simeo Makoba.

Mzee Furaha Lukeyemba akiwa katika picha ya pamoja na team nzima iliyofika nyumbani kwake mtaa wa Chamaguha kumpatia msaada.
Kutoka Kushoto ni Jirani Hirsi Mohamed ambaye ni jirani wa Mzee Furaha,Mwenyekiti wa wenyeviti Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa wa Miti Mirefu Nassoro Waryoba,Mwenyekiti wa mtaa wa Chamaguha bw. Hussein Ramadhan,Afisa Ustawi wa Jamii Manispaa ya Shinyanga Bw.Emanuel Ng'habi,Mwandishi wa Habari na Mtangazaji wa Radio Faraja kipindi cha Michapo ya Jioni Samir Salum na Meneja vipindi msaidizi wa radio Faraja Bw. Simeo Makoba wakiwa katika picha ya kumbukumbu.Picha zote na Samir Salum & Josephine Charles.

No comments: