Kuishi na mwenza siyo rahisi jipange!

JUMAMOSI nyingine tunakutana kwenye darasa la mahusiano. Maisha yetu hayawezi kwenda bila ya kuhusiana, lazima tushirikiane, tusaidizane katika mambo mbalimbali na mwisho wa siku tunatengeneza uhusiano mzuri.  Waswahili wanakuambia ili maisha ya mahusiano yawe mazuri lazima uwe na mtu sahihi ambaye atakuwa pamoja na wewe katika shida na raha. Atakayejua thamani yako wakati ambao upo na hata pale utakapokuwa haupo.

Ndiyo maana leo ninakuja na mada kama inavyojieleza hapo juu. Kuwa na mahusiano ni jambo moja lakini kuwa na mahusiano yenye afya ni jambo lingine na ndiyo maana tunashuhudia watu wengi sana wanaingia na kutoka kwenye uhusiano.

Hii inatokana na baadhi ya watu kutopenda kubeba udhaifu wa mwingine. Mtu anapokutana na mtu ambaye atamkwaza kidogo tu, akili yake inamu-ambia aingie mitini. Haoni sababu ya kubeba tatizo fulani kichwani kwake kwa muda mrefu.

Ndugu zangu lazima tuelewe kwamba kwenye maisha ya uhusiano wanakutana watu wawili ambao wamekuwa na kulelewa kwenye makuzi tofauti. Mnakutana pamoja na kuanzisha maisha mapya hivyo lazima mkubaliane katika kuvumiliana.

Unaweza kuona wewe jambo fulani unalifanya ni la kawaida kabisa lakini kumbe kwa upande wa mwenzako likawa linamkera. Analiona ni tatizo ambalo linamsumbua nafsi yake wakati wewe unaona ni jambo la kawaida hivyo usipojiongeza kwa kumsoma mwenzako basi utaendelea tu kumkera bila kujua.

Kuna watu ni wasumbufu kwenye jambo fulani usipokuwa mvumilivu hauwezi kusonga mbele. Mathalan mwenzako pengine ni mtu wa kupenda umalaya. Haridhiki na mtu mmoja, kila anaye-muona anamtaka. Anaweza kuwataka hata ndugu zako wa karibu. Kuna wengine wao tabia zao mbaya tu, hawajui suala la ukarimu, wanakuja wageni hajui hata namna ya kuwakaribisha.

Kuna wengine ni walevi wa kupindukia. Humuambii kitu kwenye suala zima la kunywa pombe, maisha yake bila pombe hayaendi. Kuna mwingine unaweza kukuta ni mvutaji wa sigara sana, ndiyo yupo hivyo kumbadilisha ni kazi kidogo. Ndiyo maana ninasema kwamba, ili uweze kuishi na mwenzako lazima uwe na uwezo wa kubeba udhaifu wa mwenzako. Usiwe mtu mwepesi wa kukata tamaa, maisha yana changamoto nyingi hivyo ni lazima uzibebe.

Simama eneo ulilopo mpaka kieleweke. Suala la msingi ni kuwa makini na kumsoma mtu pale unapoanza mahusiano. Mshirikishe Mungu katika safari yako akuoneshe mtu sahihi, mtu ambaye hatakusumbua sana katika safari yako, atakayekuelewa na mtaelewana.

Lakini pamoja na hayo, kwenye akili yako lazima ujiweke kwenye mkao wa kuvumilia. Ujue kwamba kwenye kuishi katika mahusiano, haiwezi kuwa jambo rahisi. Changamoto zipo mpya kila siku, mnaweza kuwa salama leo lakini msiwe salama kesho.

Kumbuka kwamba pindi mnapoelewana wapo maadui ambao wanaweza kujitokeza na kutaka kuharibu. Watu wa aina hii wapo tu, hauwezi kuwaepuka hivyo suala la msingi ni kujua namna ya kukabiliana nao. Kujua namna ya kuwaepuka ili wasiweze kuleta madhara katika mahusiano yenu.

Kaa tayari kukabiliana na jambo lolote litaloibuka, kuwa na moyo wa kubeba matatizo na kusamehe. Usiwe mtu wa kinyongo, muelekeze mwenzako pale unapoona anafanya jambo ambalo unaona si sahihi. Kwa kutumia lugha rafiki atakuelewa na siyo kumfokea.

Ni matumaini yangu mtakuwa mmenielewa, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii.  Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter: ENangale.

The post Kuishi na mwenza siyo rahisi jipange! appeared first on Global Publishers.

No comments: