Kocha Zahera Amtaja Litombo Yanga
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema usajili wa beki kisiki wa AS Vita ya DR Congo, Yannick Bangala Litombo ni mgumu lakini ataangalia cha kufanya, bado hajakata tamaa. Zahera ambaye ameanza kuisuka Yanga mpya huku akitarajiwa kupewa Sh.Mil 80 wikiendi hii kama advansi ya usajili amekiri kwamba Vita wanakomaa na Litombo. Litombo anacheza nafasi ya beki wa kati kwenye kikosi cha Vita ambacho kilifungwa na Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kutolewa.
Zahera ameliambia SpotiXtra linalotoka kila Alhamisi na Jumapili, kuwa mpaka sasa ameshaandaa orodha ya usajili mpya wa Yanga ambao utakuwa kabambe.
Kocha huyo anasema uswahiba wake na viongozi wa Vita pamoja na Kocha wao, Florent Ibenge ndio unamfanya asite lakini timu hiyo inamtegemea sana mchezaji huyo jambo ambalo linaweza kuigharimu Yanga. Alisema kwamba mchezaji huyo ana ushawishi mkubwa mpaka kwa mashabiki kutokana na uwezo wake uwanjani.
“Mpaka sasa nimeshaandaa orodha ya wachezaji ambao nahitaji kuwasajili na katika usajili tutakaoufanya tunaamini Yanga kwa msimu ujao itakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na aina ya wachezaji watakaosajiliwa.
“Tumekuwa tukimfuatilia Yannick Bangala ili aje Yanga lakini kwa kuwa Mwenyekiti wa AS Vita ni ndugu yangu nimeshindwa kumsajili kwa kuwa ni mmoja wa wachezaji wenye nguvu ya ushawishi na uwezo mkubwa. “Uongozi wake umeshindwa kumuachia sababu ni tegemeo sana katika timu yake hiyo lakini bado hatujashindwa,” alisema
Kocha Zahera ambaye amechukua uraia wa Ufaransa. Kocha huyo amewaambia Yanga kwamba anataka kusajili wachezaji wanaozungumza Lugha ya Kifaransa na kwa kuanzia anataka mastaa wanne kwenye nafasi ya ulinzi, kiungo na mastraika. Kila nafasi wawili. Kuhusu ubingwa, Zahera amesema kama ligi ikichezeshwa kwa haki bila figisu zozote basi timu yake inauwezo wa kutwaa ubingwa wa msimu huu.
“Bado mwezi mmoja na nusu ligi ifike ukingoni halafu Simba bado ana michezo 16, napata mashaka sana lakini kama haki ikitendeka kila timu ikashinda kwa uwezo wake naamini msimu huu Yanga tunachukua ubingwa,” alisema Zahera.
SHERIA KAMBINI Zahera amewaonya wachezaji wake kuhakikisha wanalala mapema ifikapo saa tatu usiku ili waweze kupumzisha miili yao kutokana na baadhi yao kulala usiku wa manane. Yanga kwa sasa ipo jijini Mwanza na wameweka kambi yao katika Hoteli ya Fairmunt Belmond na leo Alhamisi watavaana na Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
“Wapo baadhi ya wachezaji ikifika usiku hawalali, wanakuwa wanazunguka, sasa nimetoa onyo kila mchezaji ikifika saa tatu aingie chumbani kwake akapumzike.
“Baada ya kumaliza mazoezi niliwaita wachezaji Tshishimbi (Papy), Tambwe (Amissi) na Kamusoko (Thabani) wawaeleze wenzao kwa kuwa wao ni kama viongozi wao wachezaji wenyewe na nikawatumia huo ujumbe, naamini kila mchezaji ukifika muda atapumzika na sitarajii kumuona mchezaji koridoni wakati ni muda wa kupumzika,” alisema Kocha huyo.
The post Kocha Zahera Amtaja Litombo Yanga appeared first on Global Publishers.
No comments: