UONGO MKUBWA WANAOTUMIA WANAUME KWENYE MAPENZI
Leo atakudanganya kuhusu hili, kesho kuhusu lile ilimradi tu akuchenge usiende kupaona anapoishi na hata kama ni kukutana, basi atapendelea mkutane kwenye nyumba za kulala wageni na kadhalika.
TUNAENDELEA na mada yetu tuliyoianza wiki iliyopita, ambapo najaribu kukufungua kichwa wewe mwanamke unayetaka kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi. Mara nyingi wanaume hudanganya na maeneo ambayo hudanganya sana, ni kama ifuatavyo:
UNAISHI NA NANI?
Hili ni swali jingine ambalo wanaume wengi hupenda kudanganya na mwanamke anapomuuliza mwanaume swali hilo, majibu ambayo anayatarajia ni kuambiwa ukweli. Hata hivyo, wanaume wengi hujibu kwa urahisi tu kwamba ‘naishi mwenyewe’, ‘nimepanga mwenyewe’ au ‘naishi kwangu’.
Hata hivyo, wengi huwa wanadanganya, unaweza kukuta mwanaume anaishi na mkewe au mwanamke mwingine lakini kwa sababu anahitaji kukidhi haja za mwili wake, ataku danganya.
NAOMBA NIKAPAJUE UNAPOISHI!
Ili awe na uhakika na wewe, mwanamke kabla hajakukabidhi
moyo wake kwa asilimia 100, hupenda kujua mahali unapoishi. Hata hivyo, kwa sababu wanaume wengi hudanganya kwamba ‘naishi peke yangu’ wakati ukweli unakuta tayari mwanaume huyo anaishi na mwanamke mwingine, danadana za kutaka kupelekwa anakoishi huwa ni nyingi sana.
UHUSIANO WAKO ULIOPITA ULIKUWAJE?
Huu ni mtego mwingine ambao wanaume huutumia vizuri sana kuwanasa wanawake. Unapomuuliza mwanaume anayehitaji kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na wewe kuhusu uhusiano wake uliopita, atakachokueleza ‘kitaziteka hisia zako’.
Wanaume ni mafundi wa kuelezea stori za kufikirika, wakijifanya eti ndiyo zilizowatokea kwenye uhusiano wao wa kimapenzi wakati kiuhalisia si kweli. “Nilimfumania mwanamke wangu ndani kwangu akiwa na mwanaume mwingine!” ni miongoni mwa uongo unaotumiwa sana na wanaume wengi.
Atakwambia ‘niligundua ananicheat’, ‘hakuwa mwaminifu’, ‘aliniumiza sana moyo wangu’ na kadhalika. Bahati mbaya kwa jinsi wanawake walivyoumbwa, wakiambiwa habari kama hizi, huwaonea huruma sana wanaume husika na kujiapiza kufanya kila kinachowezekana kuwasahaulisha machungu yao, bila kujua kwamba wanaingia kwenye mtego.
NINI CHA KUFANYA?
Unapompenda mtu, hakuna kitu kinachoweza kukurudisha nyuma, hasa kama umempenda kwa moyo wa dhati. Mwanaume anaweza kuwa na kasoro chungu mbovu lakini bado mwanamke wake akawa anampenda kwa dhati.
Kwa wanaume, ile dhana kwamba wanawake wanapenda kudanganywa, inatakiwa ifutike kwenye vichwa vyao, kama mwanamke anakupenda na wewe unampenda, mweleze ukweli! Ukimdanganya halafu baadaye akaujua ukweli, mapenzi yatapungua na mwisho mtaishia kwenye migogoro inayoweza kuhatarisha kabisa penzi lenu.
Kwa wanawake, siku zote nimekuwa nikisisitiza kwamba unapoamua kumkabidhi mwanaume moyo wako, unapaswa kuwa tayari umeshamjua vya kutosha. Mambo ya kukutana leo, kesho tayari mmeshavunja amri ya sita, ni makosa makubwa ambayo huwafanya wengi kuishia kulia. Jipe muda wa kumfahamu kwa undani huyo unayetaka kumkabidhi moyo wako, mfanye awe rafiki yako kwanza kabla ya kuwa mpenzi wako.
Ukishamjua kwa undani na ukaridhika naye kwa hali hiyohiyo aliyonayo, huwezi kuja kulia kirahisi kwenye mapenzi yenu ya baadaye! Ni hayo tu, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.
The post UONGO MKUBWA WANAOTUMIA WANAUME KWENYE MAPENZI appeared first on Global Publishers.
No comments: