JAJI KIONGOZI AHITIMISHA ZIARA YAKE MAHAKAMA-KANDA YA MBEYA: ASISITIZA UONDOSHAJI MASHAURI KWA WAKATI

Na Mary Gwera, Mahakama –Mbeya
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,  Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amehitimisha ziara yake ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Mbeya huku akitoa wito kwa Uongozi wa Kanda hiyo kutoruhusu mlundikano wa mashauri.
Akizungumza na Viongozi na baadhi ya Maafisa wa Mahakama katika kikao chake cha majumuisho ya ziara yake kilichofanyika Aprili 10, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu-Mbeya, Jaji Dkt. Feleshi aliwaelekeza Viongozi hao kuainisha mashauri yote yenye umri wa miaka mine (4) lengo likiwa ni kutoruhusu mashauri hayo kuvuka miaka mitano (5).
“Nimeridhika na suala la usikilizwaji na umalizwaji wa mashauri katika Kanda hii kupitia taarifa mbalimbali zilizotolewa, hivyo ni rai yangu kuwa mashauri yote yaliyo na umri kuanzia miaka mitatu na minne (4) yaainishwe na kufanyiwa kazi kabla hayajafikia umri wa miaka mitano (5) Mahakamani,” alieleza  Jaji Kiongozi.
Jaji Kiongozi alisema kuwa lengo la Mahakama ya Tanzania ni kutokuwa na mashauri yanayokaa kwa muda mrefu kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea huku akisema kuwa nia iliyopo mashauri yasikae zaidi ya miaka miwili (2) Mahakamani kabla ya kumalizika.
Mbali na agizo hilo, Jaji Kiongozi aliwasisitiza Wahe. Majaji, Wasajili, pamoja na Mahakimu kuheshimu nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wa Mhimili huo kwa ustawi bora wa uondoshwaji wa mashauri.
Aidha;  Jaji Kiongozi alionyesha kufurahishwa kwake na juhudi za Majaji na Mahakimu wanaochapa nakala zao za hukumu na kuwapatia Wadaawa kwa wakati.
“Katika Kanda hii nimefurahishwa na jitihada za baadhi ya Mahakimu wanaochapa nakala zao za hukumu, hivyo nitoe wito kwa Majaji na Mahakimu ambao hawajaanza kuiga mfano huu ili kutopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri,” alieleza Jaji Kiongozi.
Kwa upande mwingine, Jaji Dkt. Feleshi aliagiza Mahakama katika Kanda hiyo kuhamasisha wanafunzi katika shule za Sekondari kusoma masomo ya sheria ili kuwajengea upendo wa fani ya uanasheria/uhakimu. 
Kabla ya kuhitimisha rasmi ziara yake katika Kanda hiyo, Jaji Kiongozi alitembelea na kupata taarifa za utendaji za Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Mwanzo Uyole, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Wilaya Mbeya ambapo sehemu zote Jaji Kiongozi alionyesha kuridhishwa na kasi ya uondoshaji wa mashauri na kusisitiza kuendelea na kasi hiyo.
Jaji Kiongozi amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Iringa na Mbeya lengo likiwa ni kujua  hali ya maendeleo ya utekelezaji wa maboresho ya huduma mbalimbali za  Mahakama na vilevile kuwakumbusha Watumishi wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki nchini kwa ubora wa hali ya juu kwa manufaa ya wananchi. 

 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,  Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (aliyesimama) akizungumza na Wahe. Majaji wa Mahakama Kanda ya Mbeya (pichani) pamoja na baadhi ya Viongozi na Maafisa wa Kanda hiyo (hawapo pichani) alipokuwa katika kikao cha Majumuisho ya ziara yake katika Kanda hiyo. Wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Jaji Robert Makaramba, wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Jaji Dunstan Ndunguru na wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya,  Jaji Dkt. Lilian Mihayo Mongella.
 Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Mwanzo Uyole, Zawald Nyekelela akimkabidhi Jaji Kiongozi taarifa ya hali ya Utendaji wa Mahakama hiyo pindi Jaji Dkt. Feleshi alipotembelea katika Mahakama hiyo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
 Jaji Dkt. Feleshi (katikati) akizungumza na wateja wa Mahakama (hawapo pichani), kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Jaji Robert Makaramba na kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Bw. Moses Mwidete.
 Wateja waliofika kupata huduma ya Mahakama Kanda ya Mbeya wakimsikiliza Jaji Kiongozi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao, amewasihi wananchi kuendelea kuwa na imani na Mahakama kwani ipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi.


Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania,  Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji pamoja na Maafisa wa Mahakama Kanda ya Mbeya na baadhi ya Maafisa alioambatana nao katika ziara yake ya kikazi.
 Jaji Kiongozi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Watoto iliyopo mkoani Mbeya na Maafisa wengine wa Mahakama Makao Makuu na Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, wa tatu kulia ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Zawadi Laiser.

No comments: