Halmashauri zisizotoa 10% kwa Vikundi Kukiona
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani S. Jafo(Mb) amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuhakikisha wanatoa mikopo kwa vikundi vya Vijana, Wanawake na Walemavu kutoka katika asilimia kumi ya mapato ya ndani kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake asubuhi ya Leo Mhe. Jafo amesema Halmashauri zitakazoshindwa kutoa mikopo kwa vikundi hivyo watachukuliwa Hatua kali za kisheria kama ilivyoelekezwa katika Kanuni za utoaji wa mikopo ya vikundi.
Amesema kuwa licha ya uwepo wa Sheria inayoelekeza suala zima la Utoaji wa mikopo kwa vikundi, utekelezaji wake umekua wa kusuasua sana kwa baadhi ya Halmashauri na hadi kufikia Machi 2019 jumla ya fedha zilizotolewa kwa vikundi ni shilingi bilioni 20.7 ya shilingi bilioni 54.08 zinazopaswa kutolewa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 sawa na asilimia 38.27 ya Lengo.
“Hivi sasa hakuna kisingizio chochote katika utekelezaji wa sheria hii kwani Serikali imeshatoa Kanuni, zinazoongoza utoaji wa mikopo hiyo na Kanuni hizo zimetangazwa katika Gazeti la Serikali Toleo Na. 141 la Tarehe 5 April, 2019 kwa GN. Na. 286 la mwaka 2019 kwa hiyo Mkurugenzi atakayeshindwa kutekeleza kwa ufanisi atachukuliwa hatua” alisema Mhe. Jafo.
Aliongeza kuwa katika kipindi hiki kuna Halmashauri 23 ambazo zimefanya vibaya zaidi kwa kutoa mikopo chini ya asimili 20 ya malengo.
Amezitaja Halmashauri hizo kuwa ni Nsimbo, Nyasa, Busega, Kondoa Dc, Namtumbo, Kasulu Dc, Bariadi Dc, Msalala, Mbulu Tc pamoja na Njombe Dc.
Halmashauri zingine ni Kongwa Dc, Musoma MC, Sumbawanga Dc, Kondoa Tc, Uvinza Dc, Ilala Mc, Lindi Dc, Mpwapwa Dc, Bahi Dc, Chamwino Dc, Momba Dc, Temeke Mc, Mbulu Dc na Lindi Mc.
Wakati huo huo Mhe. Jafo alitoa maelekezo kwa Halmashauri zote kuwa zinapaswa kutoa fedha kwa vikundi kwa mujibu wa Sheria na mpaka ifikapo Juni 30,2019 Halmashari ziwe zimetoa mikopo siyo chini ya asilimia 83 ya fedha zote za mikopo kutoka asilimia 10 ya fedha zote za mapato ya ndani.
Ameoongeza kuwa mpaka ifikapo Julai 20, 2019 Halmashauri zote ziwe zimetoa mikopo yote kwa asilimia 100 ya fedha zote za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Mkurugenzi yeyote atakayeshidwa kutoa fedha kwa Vikundi kama ilivyoanishwa hapaswi kumlaumu mtu yeyote kwa sababu atachukuliwa hatua kama ilivyo elekezwa kwenye Kanuni za utoaji wa mikopo ya vikundi” amesema Mhe. Jafo.
Ikumbukwe kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho katika Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura Na, 290 katika kifungu 37A ambacho kimeelekeza namna ya utoaji wa mikopo kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu kutoka katika asilimia 10 ya mapato ya ndani.
No comments: