ATE YATOA ELIMU NA MSAADA WA ‘PEDI’ KWA MABINTI SHULE YA UHURU MCHANGANYIKO DAR
Na Mwandishi Wetu, Dar
TAASISI ya Afya na Tumaini Endelevu (ATE) imetoa elimu ya afya ya hedhi kwa wasichana wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko ya jijini Dar es Salaam, pamoja na msaada wa pedi hizo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya hedhi salama duniani.
Akizungumza katika tukio hilo lililoenda pamoja na utoaji wa msaada wa pedi hizo kwa kundi hilo la wasichana wenye mahitaji maalum, Mwenyekiti wa ATE, Bi. Lilian Lema amesema wametoa elimu ya afya ya hedhi kwa wasichana hao ili iweze kuwasaidia.
“Leo tunatoa elimu kuhusu hedhi salama, usafi wa mwili wa mwanamke, na tunagawa pedi pamoja na kuhamasisha jamii kuwalinda watoto kuanzia ngazi ya familia na vitendo vyote vya unyanyasaji wa kijinsia,” alisema Bi. Lema katika ziara hiyo.
Alisema wameguswa kusaidia kundi hilo la wasichana wenye mahitaji maalumu kwa sababu mara nyingi hukumbana na changamoto katika kupata taarifa sahihi, vifaa vya hedhi salama, na mazingira yanayowajali.
Taarifa zaidi zinabainisha baadhi ya wasichana hujikuta wakikosa masomo kwa siku tatu hadi saba kila mwezi wanapokuwa kwenye hedhi kwa sababu ya kukosa ‘pedi’.
Wasichana hao hulazimika kubaki nyumbani wakihofia kuchafuka na kuaibika mbele za watu, huku wakijikuta wakikosa fursa ya kushiriki masomo na wenzao kwa kipindi hicho.
Bi. Lema alifafanua zaidi kuwa, upatikanaji wa uhakika wa pedi kwa wanafunzi wa kike wakiwemo wa shule za msingi na sekondari nchini utaimarisha elimu ya mtoto wa kike kiujumla.
"Mtoto wa kike anapokuwa na uhakika wa kupata vifaa vya kujihifadhi anapokuwa katika siku zake inampa amani ya kujifunza na kuzingatia masomo yake bila ya kuwa na wasiwasi wa kuchafuka,"alisema.





.jpeg)



No comments: