NZI CHUMA: Kutoka Taka Hadi Chakula cha Mifugo na Mazingira

 


Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
NDANI ya makasha yaliyojaa taka zinazooza katika maabara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ndaki ya Elimu (DUCE), maelfu ya funza weupe hujificha chini ya mabaki ya vyakula wakila kwa kasi.

Baada ya wiki chache, funza hao hugeuka kuwa chanzo cha protini kwa ajili ya chakula cha kuku, samaki na nguruwe huku wakisaidia kupunguza taka zinazochafua mazingira.

Huo ndio ubunifu wa watafiti wa DUCE waliobuni mradi wa kufuga black soldier fly maarufu kama nzi chuma, wadudu wanaotajwa kuwa sehemu ya suluhu ya changamoto ya chakula cha mifugo na taka ozo mijini.

Pia ubunifu huo unatajwa kuja kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga uchumi wa kisasa, matumizi ya teknolojia, uhifadhi wa mazingira na ajira kwa vijana,

Mtafiti na Mhadhiri kutoka Idara ya Kemia chuoni hapo, Dkt. Lucas Luchemba, anasema walifanya utafiti huo mwaka 2022 baada ya kuona gharama za protini kwenye chakula cha mifugo zikiendelea kuongezeka.

“Tuliangalia kwamba wadudu hawa wanaweza kutoa funza wenye kiwango kikubwa cha protini kati ya asilimia 40 hadi 50 ambazo zinafaa kwa kuku, samaki na mifugo mingine,” anasema.

Kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), funza wa black soldier fly wana kiwango kikubwa cha protini kinachowafanya kuwa mbadala wa unga wa samaki (fishmeal) na soya kwenye chakula cha mifugo.

Sekta ya mifugo nchini Tanzania imeendelea kukua sambamba na ongezeko la mahitaji ya nyama, mayai na samaki, lakini gharama ya chakula cha mifugo imeendelea kuwa changamoto kwa wafugaji wengi.

Tafiti zinaonesha kuwa chakula huchukua hadi asilimia 60 hadi 70 ya gharama za uzalishaji wa mifugo huku bei ya fishmeal na soya ikiendelea kupanda.

Utafiti uliochapishwa mwaka 2022 katika jarida la Poultry Science ulionesha kuwa funza wa black soldier fly wana kiwango cha protini kinachofikia asilimia 54.9, kiwango kinachokaribiana na fishmeal yenye asilimia 56 huku kikizidi soybean meal yenye wastani wa asilimia 47.4.

Tofauti na soya inayohitaji ardhi kubwa ya kilimo au fishmeal inayotegemea rasilimali za baharini, funza hao huzalishwa kwa kutumia taka ozo kutoka majumbani, migahawani na masokoni.

Dkt. Luchemba anasema hapo ndipo walipoona suluhu ya protini inaweza pia kuwa suluhu ya mazingira.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2020, Dar es Salaam huzalisha takribani tani 4,500 za taka kila siku huku sehemu kubwa ikiwa ni taka zinazooza.

Aidha, Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Taka Ngumu wa mwaka 2018 ulionesha kuwa taka ozo ni miongoni mwa changamoto kubwa za mazingira katika miji mikubwa kutokana na kuchangia harufu, mafuriko na uzalishaji wa methane.

Methane ni moja ya gesi zinazochochea ongezeko la joto duniani.

“Madampo mengi yanajaa kutokana na taka hizi zinazooza na kutoa harufu kali. Tukiona taka kama rasilimali, tunaweza kupata chakula cha mifugo na wakati huo huo kusaidia mazingira,” anasema Dkt. Luchemba.

Anasema tofauti na nzi wa kawaida wa majumbani, nzi chuma hawana madhara kwa binadamu kwa sababu hawana mfumo wa chakula wala midomo ya kula au kusambaza uchafu.

Safari ya kuzalisha funza hao huanza kwa kupata nzi wazazi wanaotaga mayai.

Dkt. Luchemba anasema nzi hao huwekwa kwenye neti maalum zenye majike na madume ambao hupandiana na kutaga mayai. Harufu ya taka zinazooza huwavutia zaidi kuzaliana.

“Taka huachwa kwa siku nne hadi tano kuoza kabla ya kuwekwa mbao maalum ambazo nzi hutagia mayai,” anasema.

Mayai hayo huwekwa kwenye chombo maalum kilicho juu ya wavu huku chini kukiwa na chakula kama pumba.

Ndani ya siku mbili, mayai hutotolewa na kutoa funza wadogo.

Baadaye funza hao huhamishiwa kwenye makasha yenye taka zilizochakatwa.

“Wanajificha chini ya taka na kuanza kula. Ndani ya wiki moja wanakuwa wakubwa na wazito huku wakiwa wamekusanya protini ya kutosha,” anasema.

Kwa mujibu wake, ndani ya wiki mbili taka nyingi huwa zimevunjwavunjwa huku funza wakipatikana kwa wingi.

Katika uvunaji, asilimia 10 ya funza huachwa kwa ajili ya kuzalisha kizazi kingine huku wengine wakichakatwa kwa matumizi ya chakula cha mifugo.

“Sisi tuna maabara ambayo tunawachakata funza hawa. Tunaweza kuwakausha, kuwasaga kuwa unga laini au kuwauza wakiwa hai,” anasema.

Kwa sasa mradi huo huzalisha kilogramu 300 hadi 400 za funza katika mazingira ya chuo huku kilogramu moja ya funza wabichi ikiuzwa Sh 2,500 na waliokaushwa Sh 5,000.

Kutokana na ongezeko la gharama za chakula cha mifugo, watafiti hao wameanza kutengeneza chakula cha kuku na samaki kwa kuchanganya mahindi, pumba na unga wa funza.

“Tunalenga kupunguza utegemezi wa samaki na soya ambazo gharama zake zimekuwa kubwa,” anasema.

Wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa matumizi ya protini mbadala kama nzi chuma yanaweza kusaidia kujenga mifumo himilivu ya uzalishaji wa chakula kwa kupunguza utegemezi wa malighafi zinazoweza kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mbali na uzalishaji wa chakula cha mifugo, mradi huo pia umegeuka kuwa shamba darasa kwa wanafunzi na jamii.

Dkt. Luchemba anasema tayari wamefikia shule tano za Dar es Salaam pamoja na wanafunzi wa shahada na watu binafsi wanaotaka kujifunza ufugaji wa nzi hao.

“Tunataka kuhakikisha mafunzo ya amali yanafanyika kwa vitendo na vijana wanapata ujuzi wa kujiajiri kupitia teknolojia hii,” anasema.

Anasema ndoto yao ni kuzalisha tani 10 za funza kila mwezi ili kuwafikia wafugaji wengi zaidi pamoja na kusaidia kupunguza taka kwenye madampo.

Mradi huo umewezeshwa na COSTECH kupitia fedha za kuendeleza ubunifu pamoja na mafunzo ya biashara na umiliki wa hati miliki.

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto kubwa bado ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu matumizi ya wadudu kwenye chakula cha mifugo.

Mkazi wa Dar es Salaam, Angela Mauto, ambaye alianza kufuga nzi hao mwaka 2018 kwa lengo la kupata mbolea, anasema mwanzo watu wengi hawakuelewa kile alichokuwa akifanya.

“Mwanzoni nilipata wakati mgumu kuwaaminisha watu kuwa hiki ni chakula kizuri kwa mifugo. Wengi waliona kama uchafu tu,” anasema.

Anaeleza kuwa wakati mwingine alikuwa akifuga nzi hao ndani ya mazingira ya nyumbani jambo lililozua maswali kutoka kwa watu waliomzunguka.

“Kuna wakati nilikuwa naishi nao kabisa ndani ya nyumba. Jamii ilikuwa hainielewi kutokana na mazingira na eneo nililokuwa nafugia,” anasema.

Licha ya changamoto hizo, watafiti hao wanaamini teknolojia hiyo inaweza kuwa sehemu ya suluhu ya taka, gharama za chakula cha mifugo, ajira kwa vijana na ujenzi wa miji yenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Naye Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Richard Muyungi, anasema Tanzania huzalisha kati ya tani milioni 17 hadi 20 za taka kwa mwaka huku serikali ikiweka mkakati wa kuhakikisha asilimia 70 ya taka hizo zinachakatwa na kurejelezwa ifikapo mwaka 2050.

Amesema ubunifu wa vijana katika kuchakata taka unaweza kusaidia kufanya taka kuwa rasilimali yenye thamani kiuchumi.

Kutoka kwenye taka zinazotupwa kila siku na wengi kuziona kama uchafu, watafiti wanaona fursa ya kuzalisha chakula cha mifugo, kupunguza taka na kufungua njia mpya za ajira kwa vijana. Kile kinachoonekana kuwa mabaki yasiyo na thamani kinaendelea kupewa matumizi mapya kupitia teknolojia inayolenga kukabiliana na changamoto za mazingira na uzalishaji wa chakula.


No comments: