RAIS SAMIA: TANZANIA IMEPIGA HATUA KUBWA KATIKA USAWA WA KIJINSIA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa kupitia utekelezaji wa Ilani ya CCM, Serikali imepiga hatua kubwa katika kufanikisha malengo ya kuhakikisha kesho bora na njema zaidi kwa vijana wa Kitanzania, wa kike na wa kiume.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mwanamke, yaliyofanyika leo Jumamosi, tarehe 8 Machi 2025, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, Mhe. Rais Dkt. Samia alieleza kuwa Tanzania ina mengi ya kujivunia katika kuboresha mazingira yanayohakikisha ndoto ya usawa wa kijinsia inafikiwa nchini.

“Tunapoadhimisha miaka 30 tangu Tamko la Umoja wa Mataifa la Mkutano wa Beijing, miaka 10 ya Malengo Endelevu ya Dunia na miaka 5 ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa, ni fursa ya kutathmini mafanikio makubwa yaliyofikiwa na kutambua hatua zaidi zinazohitajika ili kuhakikisha kila msichana na mwanamke hapa nchini anapata nafasi ya kufikia ndoto zake,” alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.

Aidha, alisisitiza kuwa hatua mbalimbali za kisera na kisheria zimechukuliwa na zinaendelea kuchukuliwa ili kupambana na mila kandamizi na ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

“Watanzania, wake kwa waume, wameunga mkono maamuzi na hatua mbalimbali za kumwezesha mwanamke, hali ambayo imewezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa katika usawa wa kijinsia,” aliongeza.

Akifafanua maendeleo yaliyopatikana, Rais Dkt. Samia alitaja hatua kubwa zilizochukuliwa katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini, sambamba na Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa. Alisema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza umaskini, kukomesha njaa, kuboresha afya na ustawi, elimu bora, usawa wa kijinsia, maji safi na usafi, nishati mbadala, kazi zenye staha, ukuaji wa viwanda, ubunifu na miundombinu, pamoja na kuimarisha amani, haki na taasisi madhubuti.

“Hadi tunapofanya tathmini ya mpango wa tatu wa maendeleo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo, tayari tumepunguza umaskini kwa asilimia 26 kutoka kiwango cha awali tulipoanza utekelezaji wa dira. Leo hii, pamoja na jitihada zinazoendelea, tunakaribia kufikia asilimia 30,” alisema.

Kwa upande wa uhakika wa chakula, Rais Dkt. Samia alifafanua kuwa Tanzania imejitegemea kwa chakula kwa asilimia 128 na imefanikiwa kuondoa njaa kwa asilimia 100.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Rais Dkt. Samia aliwataka Watanzania wote—wanawake na wanaume—kuendelea kujenga jamii makini yenye maadili ya Kitanzania, kuanzia ngazi ya familia, ambayo ndiyo msingi wa taifa imara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono waandamanaji kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia Wananchi kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.

  
Matukio mbalimbali kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwaajili ya kushiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025. 

Maandamano ya Wanawake kutoka Taasisi mbalimbali za umma na binafsi yakipita mbele ya Jukwaa kuu kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha tarehe 08 Machi, 2025.

No comments: