Mahakama Yamuru Kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Benki ya NBC.

 MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, imeamuru kukamatwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Theobald Sabi, kwa kushindwa kutekeleza hukumu inayoitaka benki hiyo kurudisha hati ya umiliki wa kiwanja kilichopo Kariakoo kilichotumika kudhamini mkopo wa shilingi bilioni 3.


Jaji Lusungu Hemed alitoa amri hiyo Jumatatu Februari 17, 2025 baada ya kuridhia maombi ya utekelezaji kwa Mkurugenzi Mkuu wa NBC kukamatwa na kufungwa jela akiwa mfungwa wa madai kwa kushindwa kutii huku ya mahakama iliyotolewa takriban miaka kumi iliyopita.

"Mkurugenzi Mkuu wa Mdaiwa wa Kwanza (Benki ya Taifa ya Biashara) akamatwe na kufikishwa mahakamani hapa Machi 11, 2025 saa 9.00 asubuhi kwa ajili ya mchakato wa kuwekwa kizuizini," Jaji hemed alisema katika amri yake ya Februari 17, 2025.

Mmiliki wa kiwanja hicho, Ramadhani Massudi na Family LTD alifungua maombi ya kukazia hukumu baada ya kushinda kesi ya ardhi, ambayo hukumu yake ilitolewa na Jaji Sophia Wambura, ambaye sasa amestaafu, Julai 24, 2015, akiiagiza benki hiyo kurudisha hati ya kiwanja hicho kwa mmiliki.

Maombi hayo yalisikilizwa na Naibu Msajili Wanjah Hamza na kubaini kwamba kwa kuwa amri hiyo ni ya 2015, mahakama iliona kuwa Benki na Mkopaji Mkuu, Haji Associates (T) Ltd, wameshindwa kuonyesha sababu za kutosha kwa nini utekelezaji wa hukumu hiyo usiendelee.

Mnamo Februari 23, 2024, aliiamuru Benki hiyo kukabidhi mara moja hati ya kiwanja kilichopo Mtaa wa Ungoni ndani ya Manispaa ya Ilala kwa mmiliki, Ramadhani Massudi and Family LTD, mbele ya Naibu Msajili na Haji Associates (T) LTD imlipe Tsh 150m/- kama fidia.

Kwa vile mwenye hati hiyo hakuwa ametaja ni namna gani usaidizi wa mahakama ulihitajika kukazia hukumu hiyo ya mwaka 2015, mahakama ilimwagiza atafute ni njia ipi ingekuwa bora zaidi na kuifahamisha ipasavyo kwa mujibu wa sheria.

Kwa kuzingatia maagizo ya mahakama, Oktoba 30, 2024, mwenye hati hiyo kupitiaWakili Avodius Lutabingwa, aliwasilisha maombi ya kukazia hukunu hiyo, akiomba Mkurugenzi Mkuu wa NBC, Theobald Sabi, akamatwe na kufungwa kama mfungwa wa madai baada ya kushindwa kurudisha hati yake.

Pande zote mbili zilifika mbele ya Jaji Hemed mnamo Desemba 2, 2024 ambapo Wakili Mariam Ismail, wa NBC, aliomba mteja wake aonyeshe sababu kwa nini asikamatwe kwa njia ya hati ya kiapo. Wakili Lutabingwa hakupinga ombi hilo.

Jaji Hemed aliiamuru Benki hiyo kuwasilisha hati ya kiapo hiyo Desemba 16, 2024 na mwenye tuzo akaelekezwa kuwasilisha hati ya kiapo kinzani Januari 2, 2025. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 17, 2025 kwa ajili ya kusikilizwa.

Kesi hiyo ilipoitwa kusikilizwa Februari 17, 2025, Wakili Hamis Nkya na Africa Mazoea walifika mbele ya Jaji Hemed kwa naiba benki hiyo, huku Wakili Lutabingwa akimwakilisha mwenye tuzo na kuieleza mahakama kuwa hajakabidhiwa hati ya kiapo ambayo ilikuwa iwasilishwe na benki hiyo.

Wakili Nkya alisimama na kuieleza mahakama kuwa wameamua kutowasilisha hati ya kiapo ili kuonyesha ni kwa nini Mkurugenzi Mkuu wa NBC asikamatwe na kupelekwa gerezani kama mfungwa wa madai na kuomba aruhusiwe kufanya hivyo kwa njia ya mdomo.

Katika amri yake, Jaji Hemed alieleza kuwa mdaiwa analazimika kufuata utaratibu uliochaguliwa na mahakama na iwapo atashindwa kufanya hivyo hadi tarehe iliyopangwa na mahakama, itachukuliwa kuwa hana sababu ya kuonyesha na kujitetea.

"Katika maombi ya sasa, mdaiwa ameshindwa kuzingatia amri ya mahakama ya kuonyesha sababu kwa njia ya hati ya kiapo. Katika hali ya kesi hii, sina njia nyingine zaidi ya kukubali maombi haya,” Jaji alisema akaamua.

Mwaka 1998, Ramadhani Massudi alitoa hati yake ya kiwanja kilichoko Mtaa wa Ungoni, ili kumwezesha Haji Associates (T) LTD kupata mkopo wa kiasi cha bilioni 3 kutoka NBC. Rehani hiyo ilikuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mwishoni mwa mwaka huo mmoja, hati hiyo haikurudishwa. Massudi alimfuata Haji Associates kuuliza kulikoni, lakini akahakikishiwa kwamba hati hiyo ingerudishwa. Hata hivyo, hati hiyo haikurejeshwa kwa madai ya benki kuwa mkopo uliochukuliwa haukurejeshwa.


 

No comments: