UJENZI DARAJA JIPYA LA WAMI WAFIKIA ASILIMIA 89.02, KUANZA KUTUMIKA MWISHONI MWA SEPTEMBA, 2022
Na Said Mwishehe, Michuzi TV - Pwani
UJENZI wa daraja jipya la Wami ambalo linaunganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na mikoa ya Kaskazini umefikia asilimia 89.02 na unatarajiwa kukamilika Novemba 21 mwaka 2022.
Akizungumza leo Septemba 18,2022 mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, Meneja wa TANROAD Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage mesema hadi Septemba 18, mwaka huu ujenzi wa daraja ulikuwa umefikia asilimia 98, barabara unganishi asilimia 80.
"Kwa ujumla maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Ujenzi wa daraja jipya la Wami umefikia asilimia 89.02 na muda wa utekelezaji wa mradi ni miaka minne ambapo unatarajia kukamilika Novemba 21, mwaka huu. Mkandarasi alianza kazi rasmi Oktoba 22, mwaka 2018 na kazi inaendelea," amesema na kufafanua daraja hilo kutokana na kukamilika kabla ya muda uliopangwa awali linatarajia kuanza kutumika mwishoni mwa Septemba.
Kuhusu malipo amesema ndani ya mwaka mmoja tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani maendeleo ya mradi yamepanda na kufikia asilimia 89.02 kutoka asilimia 47 ya kazi zilizofanyika ndani ya miaka mitatu, sawa na ongezeko la asilimia 42.02 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
"Hadi sasa kiasi cha Sh. 48,676,661,404.85 kimelipwa ikijumuisha Sh. 27,786,481,025.03 ambazo zimelipwa katika mwaka mmoja wa Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan," amesema.
Akizungumzia faida za mradi huo amesema kiuchumi daraja hilo litaboresha usafirishaji wa bidhaa za viwandani kutoka mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kaskazini ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na nchi jirani ya Kenya.
Pia usafirishaji wa mazao ya kilimo na biashara kutoka mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro kuletwa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam pamoja na Bandari Kuu ya Dar es Salaam.
Aidha, amesema kwa upande wa ajira zilizozalishwa ni kwamba mradi huo umeajiri jumla ya wafanyakazi 197 ambao kati ya hao asilimia 92 ni wazawa wakiwemo watalaamu na wakawaida na asilimia nane ni watalaamu kutoka nje ya nchi.
Amesema faida nyingine ni kuongezeka kwa Pato la Taifa kwa viwanda kufanya biashara na mradi vikiwemo vya saruji, nondo na kokoto ambapo tani 6,980 za saruji zimetumika, tani 2,209 za nondo na tani 3,307 za kokote zimetumika.
Faida nyingine ni kupunguza muda wa kuvuka eneo la daraja kutokana na uwezo wa kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja. Aidha daraja hilo litavutia wawekezaji kulitumia kwa kuwa litapunguza muda wa usafirishaji na kuwahakikishia usalama wa vyombo vyao ukilinganisha lililokuwa likitumika awali.
"Mradi umesaidia watalaamu wazawa kuongeza ujuzi kutokana na teknolojia mpya ya ujenzi wa madaraja marefu inayoitwa Prestressed Concrete Box Girder -Free Cantilever Method. Teknolojia hiyo kwa hapa nchini bado ni ngeni, hivyo mafunzo hayo yatasaidia kujenga uwezo na ujuzi utakaolisaidia taifa letu baadae," amesema.
Akielezea zaidi daraja hilo, amesema una lengo la kutatua changamoto zitokanazo na daraja la zamani ambalo kwa sasa halikidhi mahitaji ya magari yanayopita kwa kuwa lilijengwa miaka 63 iliyopita (mwaka 1959) na ni jembamba lenye njia moja. Pia barabara zinazounganisha daraja hilo ziko kwenye miinuko mikali na Kona mbaya, hivyo kusababisha ajali na vifo mara kwa mara.
Amesema ujenzi wa daraja jipya la Wami unagharamiwa kwa fedha za Serikali Kuu Sh. 75, 134, 647,654.55 isiyokuwa na kodi la ongezeko la thamani (VAT). Usanifu uligharimu Sh. 852, 991,000.00, ujenzi unagharimu Sh. 67,779,453,717.55, usimamizi unagharimu Sh. 6,307,484,937.55 na fidia imegharimu Sh. 194,718,000.00.
Aidha, mradi ulifanyiwa upembezi yakinifu na usanifu wa kina na kampuni ya Intercontinental Consultants and Technocrats Pvt Ltd ya India kwa kushirikiana na Apex Engineering Co.Ltd ya Tanzania kwa gharama ya Sh. 852,991,000.00 isiyo na VAT mwaka 2016.
DARAJA LENYEWE LILIVYO
Ameongeza kuwa, daraja jipya lina urefu wa mita 513.5 kwa kutumia teknolojia ya madaraja marefu ambapo kuna nguzo kuu nne kati ya hizo mbili zikiwa na urefu wa mita 19.6 na mbili zingine mita 37.44.1 wakati umbali kutoka katikati ya kila nguzo ni mita 120 na kutoka nguzo za pembezoni na kuta za mwanzo na mwisho wa daraja ni mita 75.
Pia, daraja lina upana wa mita 11.85 ambapo kutakuwa na njia mbili za magari za mita nne kila moja, njia mbili za waenda kwa miguu za mita 1.5 kwa kila moja na mita 0.425 za kingo za pembeni ya daraja kwa pande zote."Daraja litakuwa na taa za mionzi ya jua zenye kamera 21 zikiwekwa umbali wa mita 25 kila upande.
"Ujenzi wa barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 3.8 ambapo kilomita 2.1 upande wa Chalinze na kilomita 1 .7 upande wa Segera kwa kiwango cha lami yenye njia mbili zenye jumla ya upana wa mita 12 ambapo mita 3.5 kwa kila njia yapitayo magari, mita 2 za bega la lami na 0.5 za bega lisilo la lami kila upande," amesema Mhandisi Mwambage.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage akitoa taarifa fupi kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alipotembelea ujenzi wa daraja la Wami leo Septemba 2022 mkoani Pwani,Pichani kati ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakar Kunenge.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-PWANI.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akiwa na viongozi, wana CCM na wataalamu akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage kuhusu Daraja la Wami mkoani humo alipotembelea ujenzi wa daraja hilo leo Septemba 2022 mkoani Pwani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge wakati alipotembelea ujenzi wa daraja hilo leo Septemba 18,2022 mkoani Pwani,pichani kulia ni Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa huo Mhandisi Baraka Mwambage.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani,Mhandisi Baraka Mwambage kuhusu Daraja la Wami mkoani humo alipotembelea ujenzi wa daraja hilo leo Septemba 18,2022 mkoani Pwani,pichani kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge.PICHA ZOTE NA MICHUZI JR-PWANI.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka akizungumza na viongozi, wana CCM na wataalamu wakati alipotembelea ujenzi wa Daraja la Wami leo Septemba 18,2022 mkoani Pwani.
Katibu Wa Itikadi Na Uenezi CCM Ndg. Shaka Hamdu Shaka ,Wananchi na Baadhi ya Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wakipita katika njia ya Watembea kwa miguu Kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja jipya la Wami ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 89.02 na zaidi ya Sh. bilioni 75 zimepangwa kutumika.
No comments: