WAZEE NA CHANJO YA UVIKO-19

 

Na Joseph Lyimo
WAZEE wa Tanzania kila mwaka huungana na wazee wenzao duniani ifikapo Oktoba mosi kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wazee duniani iliyoanzishwa na baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 14 Desemba 1990.

Maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Vienna wa mwaka 1982 kwa ajili ya wazee duniani, “The Vienna International Plan of Action on Ageing” ulioboreshwa tena na mkakati wa Madrid, Hispania wa mwaka 2002.

Ili kuweza kupambana na changamoto za wazee katika karne ya 21 na kuendelea mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa ajili ya wote hivyo maadhimisho ya siku ya wazee duniani ni moja kati ya jitihada za baraza kuu la Umoja wa Mataifa (UN) katika kutambua na kuhamasisha jamii kuweza kulinda na kutetea haki msingi za wazee duniani.

Maadhimisho ya Mwaka huu ya wazee duniani yananogeshwa na kauli mbiu “Matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote’’ pamoja na kupatiwa elimu na kushiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.

Katika maadhimisho ya mwaka huu siku ya wazee duniani kunatarajiwa kuchukuliwa kwa hatua mbalimbali ili kuwasaidia wazee ikiwemo kuanzishwa kwa mabaraza ya wazee ya katika ngazi zote, kubaini wazee wote wenye mahitaji maalumu na kuwapatia kadi za bima ya afya ili waweze kupatiwa matibabu bila malipo.

Hii ni siku ambayo imetumika pia kwa ajili ya maboresho ya afya ya wazee sehemu mbalimbali za dunia, kwa kuwapima magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu, tezi Dume na kupatiwa huduma za msaada wa kisaikolojia sanjari na elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya janga la UVIKO-19.

Mmoja kati ya wazee wa kata ya Kibaya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, Burhani Ally (70) ambaye ni mkulima anasema kuwa pamoja na kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 bado kuna haja ya kuendelea kuboresha huduma ya afya, elimu, lishe, kipato na makazi kwa wazee wengi, ili waweze kuishi kwa amani.

“Pamoja na kuishi kwa furaha na utulivu na napenda kuwaasa wazee wote kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata chanjo ya Uviko-19 katika maeneo mbalimbali ya vituo vya kutolea huduma hiyo,” anaeleza mzee Ally.

Anasema kuwa pamoja na kuwataka wazee kujitokeza kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 pia anawasihi wazee kujiandaa kwa ajili ya ujio wa zoezi la sensa ya watu na makazi, zoezi ambalo linategemewa kufanyika mwezi Agosti 23 mwaka 2022.

“Tupo kwenye mchakato wa wazee kushiriki kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ila wazee tusisahau kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi ili kufanikisha ustawi wetu kwa serikali yetu kutambua idadi yetu,” anaeleza mzee Ally.

Anasema kwamba anatarajia wazee wa Wilaya ya Kiteto kwa umoja wao watashiriki ipasavyo kupata chanjo ya UVIKO-19 na pia kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi ili idadi ya wazee na jamii nyingine watambulike.

“Wazee tuna kauli mbiu yetu ya matumizi sahihi ya kidigitali kwa ustawi wa rika zote, hivyo wazee wenzangu kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye zoezi la chanjo ya UVIKO-19 Katika vituo vyetu mbalimbali vya kutolea huduma za afya,” anasema mzee Ally.

Mzee Lisiamu Mollel (65) ambaye ni mkazi wa kata ya Langai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, anayejishughulisha na ufugaji anaeleza kuwa anaipongeza Serikali kwa namna ambavyo inawapa kipaumbele wazee katika kupatiwa chanjo ya UVIKO-19.

“Wataalam wa afya wanatueleza kuwa sisi wazee ndiyo tupo kwenye nyakati ngumu kweli kweli katika kupata maambukizi ya UVIKO-19 kupitia magonjwa mbalimbali nyemelezi yanayotukumba,” anasema mzee Mollel.

Anasema kutokana na Serikali kuwajali kwa kuhakikisha kuwa wanapatiwa chanjo ya UVIKO-19 na wazee wakashiriki kupata imesababisha kutokuwepo kwa visa vya maambukizi ya janga hilo kwa wazee wa eneo hilo.

“Wazee hawakuwa wabishi katika kupata chanjo ila awali mwaka 2020 ilitokea wazee watatu wa maeneo ya karibu na hapa kwetu walipata changamoto ya kupumua ila kutokana na kuweza kupata chanjo ya UVIKO-19 hawakupata madhara makubwa kwani walipona,” anasema mzee Mollel.

Hivi karibuni ofisa wa kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, John Haule alitembelea wilaya ya Simanjiro na kuzungumza na baadhi ya wazee wa kata ya Orkesumet ikiwemo mikakati ya maadhimisho ya siku ya wazee duniani.

Haule anasema pamoja na kuhakikisha wazee wote wanaoshiriki kupatiwa elimu na chanjo ya UVIKO-19 pia watapatiwa huduma ya vipimo bure kwa wazee hao kwa magonjwa kama vile kisukari, shinikizo la damu na tezi dume.

“Kwenye maadhimisho hayo pia wazee wetu hawa pamoja na kupatiwa huduma za msaada wa kisaikolojia sanjari na kupewa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19 katika umri wao mkubwa,” anasema.

Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anaeleza kuwa wazee wapo kwenye hatari kubwa ya kupata homa kali ya UVIKO-19 kama wataambukizwa virusi vya Corona.



Dk Nzobo anaeleza kwamba homa kali ya UVIKO-19 itampelekea mzee kulazwa hospitalini, kupelekwa chumba cha wagonjwa mahututi, kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua na wakati mwingine hupelekea mzee kupoteza maisha.

Hata hivyo, anasema kuwa hatari hizo huongezeka pale mwanadamu anapofikisha miaka 50 na kuzidi kuongezeka zaidi mtu anapofikisha miaka 60, 70 na 80 hivyo wazee wanapaswa kulindwa.

Anaeleza kwamba magonjwa kama shinikizo la juu la damu, kisukari, magonjwa ya figo, yanachangia kuleta madhara makubwa ya janga la UVIKO-19 endapo mzee akipata.

Mtaalam huyo wa afya anasema kuwa watu wengi hasa wazee wenye kupata magonjwa sugu kama hayo walipata maambukizi ya UVIKO-19 na wengi wao walifariki dunia.

“Kwa maeneo ambayo mimi nimefika kuhamasisha watu kupata chanjo, watu wengi wazee na vijana wamechanja kwa hiyari yao wenyewe tena kwa idadi kubwa bila kushinikizwa baada ya kupatiwa elimu hivyo tuchanje,” anaeleza Dk Nzobo.

Anasema watu mbalimbali hususani wazee wanashiriki kupata chanjo ya UVIKO-19, ila wamebaki wachache ambao bado hawataki, japokuwa wanatumia mbinu ya kuwafuata mitaani ili kuwaelimisha kwa kila kundi la jamii na wanajibu maswali yao.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akizungumza Agosti 10 mwaka 2022 kwenye ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan Mkoani Njombe, anasema janga la UVIKO-19 bado lipo hivyo watanzania na wazee waendelee kupata chanjo ili kujikinga na kupambana.

Waziri Ummy anaeleza kwamba hadi hivi sasa watanzania milioni 15.5 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea sawa na asilimia 50.53 ya walengwa waliopaswa kupata chanjo wameshiriki kupatiwa chanjo ya UVIKO-19.

“Ujanja ni kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani hata ukikumbwa na janga hilo ukiwa umeshapata chanjo hautapambana kwa kutumia nguvu nyingi, tofauti na mtu ambaye hakupatiwa chanjo,” anamalizia kwa kusema Waziri Ummy.

No comments: