TANZANIA YAANDAA ALL AFRICA CHALLENGE TROPHY KWA MARA YA KWANZA

 








Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA inatarajia kuwa mwenyeji wa mashindano ya All Africa Challenge Trophy, ambayo ni mashindano ya golf kwa ajili ya wanawake na itajumuisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 20 kutoka Afrika.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Rais wa Tanzania Ladies Golf Union (TLGU) Sophia Viggo alisema wanajivunia kama Umoja wa wanawake wacheza golf na Tanzania kwa ujumla, kupata fursa ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa ambayo yamekuwa yakifanyika kwa miaka 30 sasa na kufanyika kila baada ya miaka miwili.

“Tumekuwa tukishiriki katika mashindano yote yaliyopita na tunaYyo furaha kuwa mwenyeji mwaka huu. Tunaishukuru Wizaya ya Utamaduni na michezo kwa kupitia Baraza la Michezo Tanzania,” alisema.

Alisema Mashindano hayo yatafanyika katika Viwanja vya Gymkhana Septemba 6, 7 na 8 , 2022 ambapo zawadi zitatolewa Septemba 8, 2022 mara tu baada ya mashindano kumalizika.

Alisema washiriki wanatarajiwa kuanza kuwaili kuanzia Septemba 2, 2022 kisha watafanya mazoezi Septemba 4 na 5, 2022 kabla ya ufunguzi rasmi utakaofanyika Septemba 5, 2022 jioni.

Kwa mujibu wa Rais huyo nchi shiriki ni pamoja na Tanzania, Nigeria, Botswana, Malawi, Uganda, Togo, Rwanda, Zimbabwe, Afrika Kusini, Kenya, Namibia, Senegal, Ghana, Burkina Faso, Morocco, Tunisia, Mali, Zambia, Ivory Coast, Mauritius, Gabon, Misri, Sierra Leone na Cameroon.

“Tunatarajia kutetea kombe hili ambalo tulishinda katika mashindano yaliyopita yaliyofanyika nchini Ghana mwaka 2018 ambapo mwenzetu, Madina Idi, ambaye ni Katibu wa TLGU alikuwa mshindi wa jumla,” alisema na kuongeza kuwa mwaka 2020 mashoinado hayo yalitakiwa kufanyika nchini Namibia lakini haikuwezekana kwa sababu ya UVIKO-19.

Katika hatua nyingine, Bi. Viggo alisema mara baada ya mashindano hayo, wamepanga kufanya mashindano mengine ya Tanzania Ladies Open yatakayofanyika Septemba, 10, 11 na 12, 2022 na yatatanguliwa na mazoezi Septemba 9, 2022.

“Haya ni mashindano ya Kitaifa lakini tuliamua kuunganisha na All Afrifa Challenge Trophy ili kuruhusu washiriki pia waweze kushindana katika Tanzania Ladies Open,” alisema na kuongeza kuwa itakuwa wiki nzima ya golf.

Aliwashukuru wadhamini wa mashindano hayo ambao ni pamoja na Serengeti Breweries Limited (SBL), Great Lakes, Pepsi, Oryx, Prima Afro, National Internet Data Centre (NIDC), Garda World, Mohamed Enterprises Tanzania Limited (METL), Wadsworth, Freight & Transport, Capital Finance Ltd, Cornerstone Solutions Ltd na Savvy Fm.

No comments: