NMB yazindua ATM ya kubadili fedha za kigeni uwanja wa KIA


Benki ya NMB leo imezindua rasmi mashine ya kubadilisha fedha (Forex – ATM) katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) yenye uwezo wa kubadili fedha za kigeni kwenda shilingi za Kitanzania. Hii ni hatua nyingine muhimu kwa Benki ya NMB ya utoaji huduma kwa Watanzania wanaosafiri kutoka nje, watalii na wageni wanaokuja nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi uwanjani hapo, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna alisema, wateja na hata wasio wateja wa NMB sasa wanaweza kubadilisha fedha hadi kiasi cha Dola za Kimarekani 2,000 kwa wakati mmoja kwa viwango vya kubadilishia fedha vya Benki ya NMB kwa kujihudumia wenyewe kwa kutumia mashine hii ya ATM katika uwanja huo. Aliongeza kuwa, mashine hii pia inauwezo wa kubadilisha Euro za Umoja wa Ulaya na Pauni ya Uingereza kwenda shilingi ya Tanzania.

Uzinduzi huu ni muendelezo wa huduma hizo zilizozinduliwa kwa mara ya kwanza na NMB Jijini Dar es Salaam kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na Benki hiyo inatarajia kupeleka huduma hizo maeneo mengine ikiwemo uwanja wa ndege wa Kimataifa Abeid Amani Karume (AAKIA) Zanzibar na Zanzibar Stone Town.

Bi. Ruth alisizitiza kuwa, sasa watakao hitaji kubadili fedha uwanjani hapo, watajihudumia wenyewe wakati wote masaa 24/7 na wameanza na aina hizo tatu za sarafu, lakini muda sio mrefu wataongeza na fedha za mataifa mengine.

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Kiliamanjaro Mhe. Nurdin Hassan Babu aliipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha huduma hiyo muhimu kwani imesubiriwa kwa muda mrefu mkoani hapo, ikizingatiwa kuwa mkoa huo umekuwa ukipokea wageni wengi wa kigeni ambao ndio wenye uhitaji mkubwa wa kubadili fedha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) Bi. Christina Makatobe, alisema huduma hiyo ni muhimu kwa taasisi hiyo haswa ikitiliwa maanani KIA ni lango la kuingilia wasafiri kwa wingi, wengi wao wakiwa ni watalii na sasa hata wanaoingia uwanjani hapo nyakati za usiku watabadilisha fedha kwa kujihudumia wenyewe – hii itakuwa kivutio cha watalii wengi nchini kutokana na ukweli huduma bora haswa za kifedha ni moja ya vigezo ambavyo watalii hufuatilia kabla ya kutembelea nchi husika.

Bi.Christina aliiahidi kuendelea kushirikiana na NMB kuhakikisha wanaungana katika kuweka mazingira mazuri ya kuboresha sekta ya utalii nchini hasaa kupitia watumiaji wa uwanja wa KIA.


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Hassan Babu akionyesha fedha za kitanzania baada ya kubadili fedha za kigeni kwenye FX ATM ya NMB iliyozinduliwa rasmi katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna(kushoto) na Mkurugenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro - Christine Mwakatobe.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Hassan Babu akikata utepe kuashiria kuizindua rasmi mashine ya kubadilishia fedha za kigeni kwenda Shilingi za Kitanzania (FX ATM) ya NMB katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA). Kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mkurugenzi wa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro - Christine Mwakatobe na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Ndg. Juma Irango wakishuhudia.

No comments: