WAKAZI 61 WALIOSALIA MAGOMENI KOTA WAKABIDHIWA NYUMBA ZAO

Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni Kota, Bw. George Abel (kushoto) akizungumza kabla ya zoezi la kukabidhi majina ya kaya 61 zilizosalia kukabidhiwa nyumba zao awali kutokana na kuwepo na mvutano wa kifamilia.

 

Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe (kulia) akizungumza na wakazi wa Magomeni Kota kabla ya kukabidhi majina ya kaya 61 zilizosalia kukabidhiwa nyumba zao. Kaya hizo zilishindwa kukabidhiwa awali kutokana na kuwepo na mvutano wa yupi anastahili kukabidhiwa nyumba hizo.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Arch. Daud Kondoro (kulia) akizungumza na wakazi wa Magomeni Kota kabla ya kukabidhi majina ya kaya 61 zilizosalia kukabidhiwa nyumba zao awali kutokana na kuwepo na mvutano wa kifamilia.



Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe (kulia) akimkabidhi Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni Kota, Bw. George Abel orodha ya majina ya kaya 61 za wakazi wa Magomeni Kota wanaostahili kukabidhiwa nyumba zao.


Sehemu ya Wakazi wa Magomeni Kota wakiwa katika mkutano huo.




Mkuu wa Idara ya Miliki wa Wakala wa Majengo Tanzania, TBA Bw. Saidi Mndeme akizungumza na Wakazi wa Magomeni Kota kabla ya zoezi la kukabidhi majina ya kaya 61 zilizosalia kukabidhiwa nyumba zao awali kutokana na kuwepo na mvutano wa kifamilia.


SERIKALI imekabidhi nyumba 61 zilizokuwa zimesalia kwa wakazi wa Magomeni Kota ambao awali wakati familia 644 zilipokabidhiwa nyumba wao hawakupewa kutokana na mvutanokatiyao na familia, hivyo Serikali kuamua kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wamiliki halali wanaostahili kupewa nyumba hizo.

Akikabidhi majina hayo, leo jijini Dar es Salaam, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kinondoni, Bi. Stella Msofe pamoja na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania TBA, Arch. Daud Kondoro alisema familia/kaya 644 tayari zilikwisha kabidhiwa nyumba zao tangu awali, isipokuwa nyumba 61 ambazo zilikuwa na mvutano kwa umiliki na wanafamilia hivyo Serikali na TBA kuamua kufanya uchunguzi upya ili kujihakikishia waliostahili kupewa nyumba hizo.

Alisema Serikali iliamua kufanya uchunguzi wa kina kupitia timu maalum ili kujiridhisha kabla ya kuamua kukabidhi nyumba hizo zilizosalia. Alisema mvutano huo wa wanafamilia ulisababisha kutokabidhi nyumba hizo awali na kuamua kufanya uchunguzi ni nani anastahili kukabidhiwa ili kumaliza mvutano huo wa wanafamilia.

Akifafanua kwa kina kabla ya kukabidhi nyumba hizo, Bi. Msofe alisema Serikali iliamua kufanya uchunguzi kwa kuzipitia kwa kina nyaraka za wahusika, kuwahoji na kutafuta taarifa za ziada ili kupata ukweli wa suala hilo kabla ya kutoka na uamuzi huo wa kubaini wahusika halali wanaostahili kukabidhiwa kwenye mzozo huo.

Alisema familia ambao hawataridhishwa na uamuzi huo bado wanayo nafasi ya kuwasilisha madai yao na ushahidi ili yaweze kufanyiwa kazi tena kabla ya kutolewa uamuzi. "Leo tunakabidhi majina haya baada ya uchunguzi wetu na kujiridhisha kuwa orodha hii ndio wanaostahili kukabidhiwa nyumba baada ya kufanyiwa kazi na timu yetu ya wataalam waliosimamia zoezi la uchambuzi," alifafanua Katibu huyo kwa wananchi walioshiriki katika tukio hilo.

Hata hivyo, aliwataka wakazi wote wa Magomeni Kota kuanzia sasa kubeba jukumu la matunzo, usafi, umeme, ulinzi na gharama nyingine za makazi yao kwani Serikali kupitia TBA imesitisha rasmi leo kubeba gharama za huduma hizo kwa kuwa wakazi wote wamesha kabidhiwa nyumba zao.

"Nyumba hizi zinaitaji matunzo, usafi wa maeneo yanayozunguka, bustani zake, gharama za umeme na mambo mengine muhimu zote zinatakiwa kuchangiwa na wakazi wa hapa wala si Serikali. Leo mnakabidhiwa zikiwa zinapendeza kama hazitahudumiwa kama mlivyozikuta zitachakaa na mazingira hayata kuwa ya kuvutia kama ilivyo sasa," alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni Kota, Bw. George Abel akipokea orodha hiyo ya majina 61 ameishukuru Serikali ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa ukarimu wao kuamua kulifanyia uchunguzi suala hilo haraka na kutoka na majibu ambayo yatamaliza mvutano kwa familia hizo.

Aidha ameiomba ofisi ya DAS, chini ya Bi. Msofe kuwa mlezi wa wakazi hao na kusimamia akaunti ya michango ya huduma ndani ya makazi hayo ili kurahisisha usimamizi na shughuli za michango. Aliongeza wapo baadhi ya wananchi wameanza kukaidi taratibu na hata kugomea kutoa michango jambo ambalo ni hatari hivyo kuiomba ofisi ya DAS kusaidia uratibu wa zoezi hilo.

No comments: