KITUO JUMUISHI CHA MASUALA YA FAMILIA TEMEKE CHANG’ARA KIMATAIFA



· Benki ya Dunia haiamini kinachotokea

·Kasi usikilizaji mashauri inatisha

Na. Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke kinachojishughulisha na masuala ya familia kwa huduma nzuri wanazotoa kwa wananchi, hatua iliyoifanya Benki ya Dunia kutoamini kinachotokea.

Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo leo tarehe 20 Julai, 2022 alipotembelea Kituo hicho kama sehemu ya ziara yake ya kikazi ya Mahakama kukagua shughuli mbalimbali za kiutendaji, kuangalia utoaji wa haki na kuongea na watumishi.

Jaji Mkuu huyo amebainisha kuwa mara nyingi huwa anapata pongezi kwa niaba ya watumishi kutoka katika makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo Benki ya Dunia, ambayo Mkurugenzi wake aliitembelea Mahakama ya Tanzania hivi karibuni kujionea miradi mbalimbali inayotekelezwa hapa nchini kwa ufadhiri wa Benki hiyo ya kimataifa.

“Mkurugenzi wa Benki ya Dunia amewasifu sana alipotembelea hapa tarehe 17 Novemba, 2022, hakuwa na hakika kwamba yale ambayo Benki ya Dunia ilikuwa imeota, yale ambayo yameandikwa kwenye makabrasha kuwa Kituo Jumuishi, alipofika hapa akakuta ni kweli.....

“.....aliniandikia barua kwamba niwapongeze na vile vile alituma ujumbe wa twitter kwa watumishi wote wa Benki ya Dunia kuwa watakuwa wanakuja mara kwa mara kujifunza hapa kwenu,” Mhe. Prof. Juma amewaambia watumishi hao wa Mahakama Temeke.

Amesema kuwa sifa nzuri anazozipokea hazitoki nje ya nchi tu bali pia kwa Watanzania ambao wameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi mzuri na uliotukuka kutoka kwa watumishi wa Kituo hicho cha aina yake katika Bara la Afrika.

Jaji Mkuu alinukuuu ujumbe uliotolewa na Mtanzania mmoja ambaye amewataja kwa majina ambao ni Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Mhe Ilvin Mugeta na Naibu Msajili Mary Moyo kwa kumwonyesha utendaji uliotukuka, upendo na moyo wa huruma, hatua iliyochagiza shauri lake la mirathi kumalizika kwa wakati.

Akizungumza na watumishi katika Kituo hicho, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa mafanikio waliyonayo ni mafanikio ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania kwa ujumla huku Mahakama ya Tanzania ikiwachukulia wao kuwa ndiyo chanzo cha mafanikio hayo makubwa.

“Hivyo ninawashukuru sana kwa kuweza kubeba mafanikio (haya kwa) Benki ya Dunia, Serikali na Mahakama kwa ujumla. Kwa kweli mmefanya kazi kwa mafanikio makubwa sana, hasa katika maeneo ambayo Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania inaona yanahitaji msukumo wa utoaji haki kama kesi zinazohusu talaka, mirathi na watoto zinazogusa jamii ambayo ni wanyonge zaidi,” amesema.

Kabla ya kuongea na watumishi hao, Jaji Mkuu alipata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo chumba maalumu ambacho kimetengwa kwa ajili ya akina mama kuwawezesha kunyonyesha watoto wao wachanga wanapofika katika Kituo hicho kupata huduma za utoaji haki.

“Hiki ni chumba ambacho Mtendaji Mkuu wa Mahakama alikuwa anasema ni nchi ya Ufaransa tu ndiyo wanachumba cha kunyonyeshea watoto. Katika Bara la Afrika ni (Tanzania pekee wanahuduma hii), hivyo ni sehemu muhimu na tutaendelea kuiboresha ili itoe huduma bora zaidi,” amesema.

Akizungumza katika kikao hicho, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, ambaye aliambatana na Jaji Mkuu katika ziara hiyo alishindwa kuficha furaha yake kufuatia taarifa nzuri iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho kuelezea shughuli mbalimbali za kiutendaji ambazo zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

“Nina neno moja kwa wote wanaohudumu katika Kituo hiki; hongera sana. Hapa kwa maoni yangu, ile safari ambayo unaizungumzia na kuelekeza kuwa tuianze, Kituo hiki hakijaanza kwa maneno. Safari ya kuelekea Mahakama Mtandao imeonekana na mimi kwa mara ya kwanza nimepata matumaini makubwa sana. Nafahamu changamoto mnazokabiliana nazo hasa katika kasi ya usikilizaji wa mashauri. Hali ilivyokuwa kwa miezi miwili iliyopita ni tofauti na sasa,” alisema.

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliyeambatana na Jaji Mkuu kwenye ziara hiyo ameahidi kushughulikia changamoto ndogondogo zinazokikabili Kituo hicho katika kutekeleza majukumu yake ili nyota yake ya kiutendaji iendelee kung’aa sio Tanzania pekee bali pia katika Bara la Afrika na Dunia nzima.

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Kituo hicho, Mhe. Mugeta alimweleza Jaji Mkuu kuwa tangu kilipoanzishwa tarehe 27 Agosti, 2021 hadi kufikia jana tarehe 19 Julai, 2022, mashauri 4,687 yamesajiliwa katika ngazi zote za Mahakama na asilimia 68 yamesikilizwa na kuamuliwa.

Amesema kati ya mashauri yote yaliyosajiliwa, asilimia 62, yaani mashauri 2,911 ni ya mirathi ambapo asilimia 82 ya mashauri hayo tayari wasimamizi wa mirathi na watekeleza wosia wameteuliwa na kuthibitishwa, mtawalia.

“Hadi kufikia Julai 19, 2022 jumla ya mashauri 424 yalihusisha malipo ya fedha na 15,413,629,678/63 ziliwekwa katika akaunti ya mirathi ya Mahakama. Asilimia 91 ya kiasi hiki kimelipwa kwa wanufaika kupitia mashauri 371. Bakaa iliyopo kwenye akaunti hadi tarehe ya ripoti hii ni Tshs 1,321,830,690/22 ambayo ipo katika hatua za malipo,” amesema.

Mbali na Jaji Kiongozi na Mtendaji Mkuu, viongozi wengine kutoka Makao Makuu walioambatana na Mhe. Prof. Juma katika ziara yake ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, ambaye ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHEMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Mtendaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu Bi. Maria Itala na Afisa Utumishi, Bw. Jeofrey Mnemba.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke alipofanya ziara ya kikazi leo tarehe 20 Julai, 2022 na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akichombeza neno la shukurani kwa watumishi hao.

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe Ilvin Mugeta akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mahakama hiyo.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa neno katika mkutano huo.



Afisa Tehama katika Kituo hicho cha Temeke, Bi Amina Said akifurahia jambo baada ya kuwasilisha taarifa yake kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.



Viongozi waandamizi wa Mahakama kutoka Makao Makuu wakiongozwa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, ambaye ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Kevin Mhina (wa tatu kulia) na Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi (wa kwanza kulia) wakifuatilia matukio mbalimbali katika mkutano huo.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akipokea kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta zawadi maalumu aliyotunukiwa na watumishi wa Kituo hicho.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akionyesha zawadi hiyo kwa watumishi hao (hawapo katika picha).

Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta akimkabidhi zawadi maalumu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani katika mkutano huo.





Sehemu ya watumishi katika kituo hicho (juu na chini) wakifuatilia hotuba ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha).





Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati aliyekaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya viongozi kutoka Makao Makuu ya Mahakama. Wengine waliokaa ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (wa pili kushoto), Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi Temeke, Mhe. Ilvin Mugeta (wa pili kulia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania anayehudumu katika Kituo hicho, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto).





Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati aliyekaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke (picha mbili za juu na mbili za chini).


No comments: