Walimu 736 wa Shule za Sekondari wanaofundisha masomo ya Sayansi na Hisabati wapewa mafunzo.

Leo tarehe 3/1/2022 Mafunzo endelevu kazini kwa walimu wa shule za Sekondari wa masomo ya Sayansi (Biolojia, Kemia, Fizikia) na Hisabati yamefunguliwa rasmi katika vituo viwili vya Mikoa ya Morogoro na Tabora.

Mafunzo haya ambayo yanatekelezwa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari ( Sekondary Education Quality Improvement Program-SEQUIP) yanajumuisha washiriki 736 ambapo wamegawanywa katika vituo hivyo viwili (Morogoro washiriki 368 na Tabora washiriki 368).

Kwa upande wa Mkoa wa Morogoro ,Mafunzo hayo yamefunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Leonard Akwilapo , ambaye amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo, mbinu na umahiri wa ufundishaji na ujifunzaji wa Masomo ya Sayansi na Hisabati ili kuweza kutoa matokeo chanya kwa wanafunzi.

Dkt.Akwilapo amesema, mradi huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni, kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya Sekondari, kuweka mazingira wezeshi ya ujifunzaji kwa wasichana na kuwawezesha wasichana na wavulana kukamilisha mzunguko wa Elimu kwa kupata Elimu bora ya Sekondari.

Aidha ametumia nafasi hii kuwataka wazazi kuwapeleka shule wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Elimu ya Sekondari.
"Ni kosa la jinai kuacha watoto nyumbani waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kwa mwaka wa masomo 2022, watoto wote wanapaswa kuwepo shule tarehe 17/01/2022 wazazi tekelezeni jukumu lenu."Amesema.

Aidha, katika kituo cha mafunzo cha Mkoa wa Tabora, Naibu Katibu Mkuu Elimu,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR -TAMISEMI) Bwana.Gerald Mweli katika ufunguzi wake amesema kuwa, mafunzo hayo ni mahususi katika kuhakikisha walimu wanaweza kuboresha ufundishaji wao hasa katika mada zenye changamoto katika utekelezaji wa Mitaala ya Elimu ya Sekondari.

Vile vile washiriki wa mafunzo wametakiwa kuzingatia mafunzo hayo kwa kuwa wanategemewa kwenda kuwafundisha walimu wengine katika ngazi ya KLASTA kwa lengo la kukamilisha idadi ya jumla ya walimu 5000 katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TET Dkt.Aneth Komba amesema, walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wanajengewa uwezo wa kitaalamu na kupewa mbinu za ufundishaji,TET kwa kushirikiana na Wizara na Ofisi ya Rais- TAMISEMI imeanza kwa kutoa mafunzo kwa washiriki wachache ambao watatumika kama wawezeshaji wa Kitaifa katika kuendesha mafunzo endelevu kwa walimu kazini katika KLASTA zitakazoundwa katika ngazi za vituo vya mafunzo ya walimu (TRCs) na shule katika halmashauri zao.

Amesema TET kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu imeandaa miongozo mbalimbali ili kufanikisha utekelezaji wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini.Miongozo hiyo ni usimamizi wa mafunzo endelevu kwa walimu kazini, utekelezaji wa mafunzo endelevu katika ngazi ya vituo vya mafunzo ya walimu na ngazi ya shule pamoja na uanzishaji wa KLASTA za mafunzo endelevu kazini.

Hata hivyo ,Dkt.Komba amewataka walimu hao kutumia fursa hii kujaza dodoso kuhusiana na maboresho ya Mitaala ya Elimu .

Mafunzo haya ni endelevu yanatarajiwa kufanyika katika vituo vya mafunzo ya walimu katika ngazi ya shule yakiwezeshwa ma wawezeshaji rika na wawezeshaji Kitaifa.














No comments: