WAZIRI MKUU ATOA WITO KWA WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI



*Aitaka ishiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro ya ardhi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifungo na ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ishiriki kikamilifu katika kutatua migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

“Hakikisheni wafugaji wanaelimishwa na kuhamasishwa kufuga kulingana na maeneo waliyonayo. Halmashauri nazo zihamasishe ufugaji ambao hautochochea migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.”

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo (Jumanne, Septemba 7, 2021) baada ya kufungua mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Amesema sekta ya mifugo ni moja ya sekta muhimu na ya kipaumbele kwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa na lengo la kuiwezesha sekta hiyo kuchangia ipasavyo katika kuwakwamua wananchi kiuchumi na kutoa malighafi ya katika viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.

Pia, Waziri Mkuu ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa zihakikishe zinashirikiana na wadau wa sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kutenga, kupima, kusimamia na kuendeleza maeneo ya malisho pamoja na kuwahamasisha wafugaji waboreshe mifugo yao ili kuongeza tija katika uzalishaji.

“…Viongozi na Watendaji wa Serikali hakikisheni mnashirikiana kwa karibu na sekta binafsi wakiwemo wafugaji katika kuwawezesha kuwekeza na kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya mifugo ikiwemo majosho, malambo, maeneo ya malisho na visima vya maji.”

Waziri Mkuu amesema uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za mifugo uimarishwe ili kuongeza tija katika sekta ya mifugo sambamba na kuwahamasisha wafugaji kutumia mifugo bora iliyofanyiwa tafiti na kuonesha kuwa na tija zaidi.

Amesema huduma za ugani ziimarishwe kwenye sekta ya mifugo ili wafugaji wapate mbinu bora za ufugaji pamoja na kuimarisha masoko ya mifugo kwa ajili ya kuwawezesha wafugaji kuuza mifugo yao kwa bei nzuri.

Waziri Mkuu pia ametoa wito kwa jamii ya wafugaji kuacha tabia ya kuwapa watoto kazi ya kuchunga mifugo badala yake wajikite katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu bora kwa manufaa yao ya baadae.Awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki alisema lengo la mkutano huo ni kutoa nafasi kwa wadau wa sekta binafsi kufahamu kwa undani fursa zilizopo katika sekta ya mifugo, kupata uzoefu wa pamoja na kufahamu changamoto na kujadili namna ya kuziondoa.

Kadhalika, Waziri Ndaki ametoa wito kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zigharamie na kuwashirikisha wafugaji nchini wahimilishe asilimia 20 ya ng’ombe wanaostahili kuhimilishwa kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ili kufikia lengo la wizara la kuboresha mifugo milioni tano katika kipindi cha kuanzia 2020 hadi 2025.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama viatu wakati alipotembelea banda la kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited kilichopo eneo la Karanga Moshi kabla ya kufungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 7, 2021. Wa pili kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki.



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama mkanda uliotengenezwa na kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Industries Company Limited kilichopo eneo la Karanga Moshi wakati alipotembelea banda la kiwanda hicho kabla ya kufungua Mkutano wa Wadau Sekta ya Mifugo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 7, 2021. Wa pili kulia ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)






Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla wakati alipowasili kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Septemba 7, 2021 kufungua Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Mifugo.

No comments: