WAZIRI MCHENGERWA ATOA MSAADA WA MABATI 800 KWA WAATHIRIKA AJALI YA MOTO.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Rufiji ametoa msaada wa mabati 800 kwa wahanga wa ajali ya moto Kijiji cha Nyamwage Wilayani Rufiji ambapo kaya 19 zimekosa makazi baada ya moto kuteketeza nyumba zao mnamo tarehe 29 Agosti, 2021.
Waziri Mchengerwa ametoa msaada huo katika Kijiji cha Nyamwage leo alipozitembelea familia zilizoathirika na ajali hiyo ya moto kwa lengo la kuzifariji.
Mhe. Mchengerwa amesema, ameamua kutoa msaada wa bati ili kuwawezesha wahanga kuachana na nyumba za nyasi, ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari ya kupunguza athari zinatokanazo na moto.
Kwa kuzingatia umuhimu wa elimu, Mhe. Mchengerwa amesema mara baada ya ajali hiyo ya moto kutokea, Serikali iliamua kuchukua hatua za haraka kwa kuwapatia sare za shule watoto 20 pamoja na madaftari na penseli ili watoto hao waendelee kupata elimu.
Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa kwa niaba ya Wadau wa Maendeleo Kampuni ya Lake Oil amekabidhi msaada wa chakula, magodoro, mavazi na vifaa vya shule kwa wahanga wa ajali hiyo ya moto.
Mmoja wa waathirika wa ajali hiyo ya moto, Bi. Zainabu Kapilima ameshukuru kwa kitendo cha watoto wake watatu kupatiwa msaada wa sare za shule na madaftari.
Naye, Bw. Abdallah Sango amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kuwapatia msaada wa bati zitakazowawezesha kujenga nyumba bora na kutoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwasaidia tangu waathirike na ajali ya moto.
Akizungumza kwa niaba ya wahanga na wakazi wa Kijiji cha Nyamwage, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mhe. Juma Ligomba amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa kutoa msaada wa bati ambao utaboresha makazi ya wanakijiji hao baada ya kuathiriwa na ajali ya moto kutokana na idadi kubwa ya nyumba zao kuwa za nyasi.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kutoa misaada kwa wahanga wa ajali hiyo ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida na kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa.
No comments: