Washindi mashindano ya taifa ya 'Sailing’ wapatikana

 

Washindi mashindano ya taifa ya 'Sailing’ wapatikana

Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Mashindano ya wazi ya taifa ya mchzo wa  mbio za mashua (Laser Open Sailing) yamefikia kilele juzi kwa mchezaji  Imamu Saidi wa  timu ya Dar es Salaam Yatch Club) kushinda nafasi ya kwanza.

Imamu amekusanya jumla ya pointi nane (8) kuwashinda wachezaji 38 walioshiriki mashindano hayo yaliyoandaliwa na klabu ya Dar Yatch Club na kusimamiwa na chama cha mchezo huo Tanzania TSAA. Mashindano hayo yalishirikisha klabu tatu ambazo ni Dar Yatch Club, Msasani na Kigamboni.

Mchezaji huyo ambaye alishindania daraja 4.7 (Class 4.7) alipata pointi moja katika hatua ya kwanza, pili, nne, tano na saba huku akikusanya pointi mbili katika hatua ya tatu na pointi tatu katika hatua ya sita kuibuka mshindani katika mashindano hayo ambayo yalikuwa na ushindani wa hali ya juu.

Mshindi wa pili katika mashindano hayo alikuwa Hamis Mohamed wa Dar Yatch Club   aliyepata pointi 18 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Halife Mpondi wa klabu ya Kigamboni kwa kupata  pointi 24 na nafasi ya nne ilichukuliwa na Vedastus Alphonce aliyepata pointi 26. Nafasi ya tano ilikwenda kwa Mussa Mpondi.

Akizungumza mara baada ya mashindano kuisha, Imamu alisema kuwa mashindano yamekuwa magumu na kuwapongeza waandaaji wa mashindano hayo, Dar Yatch Club chini ya katibu wake, Anna Nyimbo. “Ushindani ulikuwa wa hali ya juu na kwa kweli kuna maendeleo makubwa ya mchezo huu,” alisema Imamu ambaye ameshinda taji hilo kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Kwa upande wake, Nyimbo alisema kuwa wamefurahishwa na viwango vya wachezaji wa mchezo huo ambayo ni matunda ya mafunzo yao.

“Tumekuwa tukiendesha mafunzo ya watoto wadogo kwa kipindi kirefu nampaka sasa tumefanikiwa kupata wachezaji wazuri ambao pia wameweza kuiwakilisha nchi kimataifa,” alisema Nyimbo.

Mwenyekiti wa Chama cha mchezo huo nchini, Philimon Nasari alisema kuwa malengo yao ni kuona vijana wengi wa Tanzania wanajifunza na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa. “Mpaka sasa kuna vijana ambao wameshindana kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa Afrika na Dunia. Mwamko umekuwa mkubwa na tunaamini tutafikia lengo,” alisema Nasari.

 Imamu Saidi ambaye ni mshindi wa kwanza akishindana katika mashindano ya klabu bingwa ya Mashua yajulikanayo kwa jina la Laser Open

 Washindani wakishindana katika mashindano ya klabu bingwa ya Mashua yajulikanayo      kwa jina la Laser Open

Washindi wa mashindano ya Mashua na maofisa katika picha ya pamoja.

 



 

No comments: