VIJANA HALMASHAURI YA LUSHOTO WAPEWA ELIMU KUHUSU STADI ZA MAISHA
VIJANA waelimishaji rika wilayani Lushoto wamepatiwa mafunzo ya stadi za maisha kwa lengo la kuwezesha kundi hilo la vijana kutambua wao ni nani, wanatarajia kufika wapi katika maisha yao na jinsi watakavyofika huko wanapotarajia kufika.
Mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya vijana hapa nchini yametolewa kwa vijana waelimishaji rika 40 katika ukumbi wa Usambara, Lushoto ambapo vijana hao wamepatiwa stadi za kujitambua, kuwa na uthubutu, kuweka malengo yanayopimika na kufanya maamuzi sahihi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya Stadi za Maisha kwa waelimishaji rika katika Halmashauri ya Lushoto Mkoani Tanga Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Prof. Jamal Katundu alieleza uwepo wa sababu mbalimbali zinazowafanya vijana kutokushiriki kikamilifu katika jitihada za kukuza uchumi wa nchi mojawapo ni vijana wengi kutokuwa na stadi za maisha hali inayopelekea wao kufanya maamuzi yasiyo sahihi kama vile kujihusisha na tabia za rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu na maadili yasiyokubalika katika jamii.
“Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu katika kutambua mchango mkubwa wa vijana katika kukuza uchumi wa nchi kwa ajili ya maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla ilianzisha Programu ya Stadi za Maisha ili kuwawezesha vijana ambao ndio nguvukazi ya taifa kupata stadi za kujitambua. Hivyo ili kufikia azma hii kila kijana anapaswa kujiuliza maswali matatu ya msingi ambayo ni: Mimi ni nani, Nataka kwenda wapi maishani na Nitafikaje ninapotaka kwenda,” alieleza Katundu
“Majibu ya maswali haya yatatokana na kijana mwenyewe kwa kuwa na fikra bunifu na fikra yakinifu,” alisema
Aliongeza kuwa kupitia programu ya stadi za maisha, Mwaka 2009 Serikali iliandaa Mwongozo Sanifu na kuweka viwango stahiki vitakavyotumika katika kutoa elimu na taarifa sahihi za stadi za maisha kwa lengo la kuhamasisha mabadiliko chanya ya tabia kwa vijana. Mwongozo huu Sanifu wa Stadi za Maisha umetumika katika kuwaandaa Wawezeshaji Kitaifa wa Stadi za Maisha 78 nchi nzima, kwa maana ya idadi ya wawezeshaji watatu kwa kila Mkoa. Kupitia wawezeshaji hawa jumla ya Waelimishaji Rika 16,390 wamefikiwa na kujengewa uwezo.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa Ripoti ya Makadirio ya Idadi ya Watu kwa Mwaka 2013-2035 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakadirikiwa kuwa ifikapo Mwaka 2025 idadi ya vijana itafikia 38.3%, hivyo, kuna umuhimu wa kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha kuwa vijana hawa wanaendelezwa, wanawezeshwa na kuimarishwa katika kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za ukuzaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo alitoa wito kwa vijana wote nchini kuhakikisha kuwa wanachangamkia fursa zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha kuwa wanakuwa wepesi wa kutafuta taarifa. Sambamba na hayo amewasihi vijana kuwa wazalendo, wenye maadili na kufuata silka za Mtanzania.
“Mtumie fursa hii ya mafunzo haya ya Stadi za Maisha kwenda kushughulikia changamoto zinazowakabili vijana wenzenu kama vile matumizi ya dawa za kulevya, VVU na UKIMWI na mimba kabla ya wakati zisizotarajiwa. Mtatakiwa kufanya kazi kwa ukaribu na waratibu katika Ngazi zote ili kupanga kwa pamoja namna nzuri ya kuendeleza elimu hii,” alisema
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Calist Lazaro ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada za kuwakomboa vijana kupitia mafunzo na elimu mbalimbali zitakazowasaidia kujitambua na kujituma ili waweze kufikia ndoto zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bw. James Kajugusi alieleza kuwa umeandaliwa mpango wa kujenga uelewa wa programu hiyo ya Stadi za Maisha kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini ili kuhakikisha kuwa stadi za maisha zinahuishwa kwenye mipango ya maendeleo ya Halmashauri.
Pamoja na hayo alieleza kuwa wamejipanga kushiriki katika vipindi vya Radio na Televisheni ili kuhabarisha umma juu ya umuhimu wa stadi za maisha na pia kuandaa vitini rafiki vya elimu ya stadi za maisha vitakavyosambazwa kwa wadau wote ili elimu hii iweze kuwafikia vijana wengi.
Nao Vijana walioshiriki mafunzo hayo walisema kuwa mada walizojifunza wataenda kuzifanyia kazi na kuhakikisha kuwa wanajukwamua na changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana. Sambamba na hayo waliahidi elimu waliyoipata wataitumia pia kuelimisha vijana wenzao ili waweze kujitambua kwa pamoja katika kushiriki kwenye ujenzi wa maendeleo ya taifa.
No comments: