MAWAZIRI 30 WA AFRIKA WAIPITISHA TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA KIMATAIFA WA 65 WA UTALII 2022
Na Mwandishi Wetu, Cape Verde.
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii (UNWTO) limeichagua Tanzania kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Utalii wa 65 wa Kanda ya Afrika utakaofanyika Jiji la Arusha Oktoba,2022.
Mkutano huo, utajumuisha Mawaziri wote wa Utalii wa Bara la Afrika huku ukitarajia kuongeza tija kwa Tanzania kwenye fursa za kukuza Utalii Kimataifa.
Akizungumza jana nchini hapa katika kisiwa cha SAL, Cape Verde, katika mkutano huo wa siku Nne mbele ya zaidi ya Mawaziri 30 wa utalii, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amewashukuru Mawaziri hao kwa kuipa heshima nchi ya Tanzania huku akiowaomba mawaziri wote wa utalii kuja kushiriki katika mkutano huo mwakani.
Katika uchaguzi huo uliowakutanisha mawaziri 30 wa utalii wa Bara la Afrika, Mawaziri hao waliridhia kwa kauli moja kuwa Tanzania ina sifa zote za kuwa mwenyeji wa mkutano huo mara baada ya Tanzania kuwa nchi pekee iliyokuwa imeonesha nia ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Kufuatia hali hiyo Tanzania inakuwa ni nchi ya kwanza kupita bila kupingwa na katika mkutano wa Kimataifa wa utalii wa 64.
Akizungumzia manufaa ya mkutano huo, Dkt. Ndumbaro amesema kufanyika mkutano huo nchini utaiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa kutangaza fursa uwekezaji katika sekta ya utalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema kitendo cha Mawaziri wote kuridhia kwa kauli moja kuwa Tanzania iwe mwenyeji wa mkutano huo ni imani kubwa ya waliyonayo kwa nchi ya Tanzania na Watanzania wote kwa ujumla.
Dkt. Ndumbaro amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini Tanzania ni hatua mahsusi kwa nchi kujitangaza kimataifa kwa vile washiriki mbalimbali duniani watahudhuria mkutano huo wakiwemo wabobezi wa utalii pamoja na makampuni makubwa ya kutangaza vivutio vya utalii kutoka nje yatatangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mambokale wa Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema utachagiza idadi ya watalii watakaoitembelea Tanzania kupitia mkutano huo.
" Tunajisikia fahari kuona ajenda yetu kama nchi ya kuja kushiriki katika mkutano huu umefanikiwa na tuna matumaini makubwa kuwa mkutano huo utatangaza vivutio vya utalii vilivyoko Zanzibar na Tanzania bara". alisisitiza Mhe. Lela Mussa.
Aidha, Katika mkutano huo Tanzania imechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti na Mipango ya UNWTO kwa kipindi cha muda wa miaka mitatu kuanzia sasa.
Naye Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurab Pololikashvili amesema katika kipindi chake cha uongozi moja ya kipaumbele chake kikubwa ni kufanya uwekezaji katika bara la Afrika ili kuongeza ajira kupitia sekta ya utalii.
Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano huo unaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ambaye ameambatana na Waziri wa Utalii na Mambokale wa Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa.
Pia Wajumbe wengine walioambatana na Mhe. Waziri ni pamoja Kamishna Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Kamishna Uhifadhi kutoka TAWA, Mabula Misungwi, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Philip Chitaunga , Balozi wa Tanzania Paris, Mhe. Samweli Shelukindo pamoja na maofisa kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) , TTB pamoja na TANAPA.
No comments: