PICHA ZA MATUKIO YA MWENGE WA UHRURU KUTOKA RUVUMA
Na Muhidin Amri,Tunduru
JUMLA ya Sh.163,362,626.25 zimetumika kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji safi na salama uliotekelezwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa katika kijiji Mkowela kata ya Namakambale wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Akizindua mradi huo,kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi, amefurahishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Ruwasa kutokana na kujengwa kwa viwango na ubora mkubwa.
Amesema, mradi wa maji Mkowela unakwenda kumaliza kabisa kero ya muda mrefu ya maji safi na salama kwa wakazi wa kijiji cha Mkowela na kuharakisha maendeleo ya wakazi hao ambao awali walilazimika kutumia maji yasio safi na salama kwa matumizi ya binadamu yaliyopatikana kwenye mito na visima vya asili.
Amewataka wataalam wa Ruwasa, kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara miradi ya maji inayotekelezwa ili kufahamu kama miradi hiyo inafanya kazi na pale inapoharibika waweze kufanya matengenezo ya haraka ili wananchi wasikose huduma ya maji katika maeneo.
Amewaomba wananchi kutunza miradi ya maji inayotekelezwa kwa fedha nyingi za Serikali na kila mmoja ahakikishe anakuwa mlinzi wa mradi huo ambao unakwenda kutatua kero na kuchochea maendeleo.
Kwa upande wake,Mhandisi wa maji wa Ruwasa wilayani Tunduru Emmanuel Mfyoyi amesema,mradi huo uliibuliwa na wananchi kutokana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ambapo Serikali kupitia wizara ya maji ilitoa fedha ili zisaidie upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wa kijiji hicho.
Amesema,lengo la mradi huo ni kuboresha huduma ya maji kwa wananchi chini ya kauli Mbiu ya kumtua Mama ndoo kichwani kwa kusogeza huduma ya maji karibu na wananchi.
Mfyoyi amesema, miundombinu ya maji iliyojengwa katika kijiji hicho ni pamoja na tenki la juu lenye ujazo wa lita 50,000,kisima cha maji kinachotumia nishati ya umeme wa Gridi,mtandao wa mabomba wenye urefu wa mita 4,200 na vituo vinne vya kuchotea maji,hata hivyo vituo vitatu vimeongezeka na kuwa na vituo saba.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wibert Ibuge,amewataka Watanzania kutambua kuwa,falsafa ya Mwenge wa Uhuru imejikita katika kudumisha Amani,upendo,utulivu na mshikamano ili kujenga Taifa lenye maendeleo.
Kupitia Mwenge wa Uhuru,Mkuu wa mkoa amewasihi Watanzania kuachana na hulka na vitendo ambavyo vitasababisha uvunjifu wa Amani iliyoasisiwa na kujengwa kwa jasho na majitoleo makubwa na Waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Karume.
Aidha amesema, mkoa kwa kushiriana na wadau mbalimbali utendelea kutoa elimu na hamasa kwa wananchi juu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na jamii huru isiyotaka na inayochukia dhambi ya Rushwa.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2021 Luten Josephine Mwambashi wa pili kushoto akiangalia miundombinu ya maji katika mradi katika mradi wa maji kijiji cha Mkowela kata ya Namakambale wilayani Tunduru ambapo Mwenge wa Uhuru umefungua mradi mkubwa wa maji safi na salama uliojengwa na wakala wa maji vijijini Ruwasa,wa kwanza kushoto meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga na kulia Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Hassn Kungu. Picha zote na Muhidin Amri,
No comments: