MKURUGENZI MALINYI APATA AJALI YA GARI
Na Farida Saidy, Morogoro
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Joanfaith Kataraiya na dereva wake wamepata ajali baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kupasuka tairi ya mbele na kupinduka katika Kijiji cha Usangule wilayani Malinyi.
Akizungumza na Michuzi Media kwa njia ya simu Mkuu wa Wilaya hiyo, Mathayo Masele alisema ajali hiyo ilimetokea Septemba 05, mwaka huu majira ya saa moja kasoro jioni. Kwa saa za Afrika Mashariki.
Masele amesema walipata taarifa ya ajali hiyo kutoka kwa mkurugenzi mwenyewe baada ya kunusurika na walifika eneo la ajali kijiji cha Usangule kilometa 25 kabla ya kufika Malinyi.
Amesema licha ya maendeleo mazuri ya mkurugenzi huyo aliyejeruhiwa zaidi miguuni na dereva aliyelalamikia kuumia mgongo na kichwa, ajali hiyo ilikuwa ni mbaya kwa tairi kupasuka na gari kupinduka na tairi kuwa juu.
"Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ilifika kwa wakati eneo la tukio na kutoa msaada wa dharura kuwanusuru mkurugenzi na dereva wake ambapo majira ya saa moja na nusu usiku tuliwakimbiza kituo cha afya cha Mtimbira kwa matibabu ya awali na kuweka mazingira mazuri eneo la ajali ili isisababishe ajali nyingine,"alisema mkuu huyo.
Hata hivyo alisema majeruhi hao wawili waihamishwa kutoka kituo cha afya Mtimbira majira ya saa tano usiku baada ya matibabu ya awali na kupelekwa hospitali ya Rufaa ya St Francis iliyopo Ifakara wilayani Kilombero kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kiafya na matibabu zaidi.
Kuhusu alikokuwa akitokea na kuelekea mkurugenzi huyo, mkuu huyo wa wilaya alisema alikuwa eneo lake la kawaida la kazi na alikuwa akirejea Malinyi kuendelea na majukumu yake ya kawaida, akitokea mjini Morogoro kwa vikao.
No comments: