BODI YA NISHATI VIJIJINI YAKAGUA MRADI WA UJAZILIZI MWANZA
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (katikati) na Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa (kulia) wakiwa wameongozana na mmoja wa wakazi wa Kitongoji cha Mwahuli, Kisesa mkoani Mwanza, John Masalu (kushoto), wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme Septemba 6, 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga akionesha nguzo zinazotumiwa na Mkandarasi kusambaza umeme katika eneo la Mandu Makaburini, wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini, Septemba 6, 2021. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi Wakili Julius Kalolo na anayefuata ni Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa.
Mkazi wa Kitongoji cha Mwahuli, Eneo la Isangijo Kisesa, wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza, Magret Komanya akimwongoza Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo kwenda kuona nyumba yake iliyorukwa wakati wa kuunganisha umeme wakazi wa eneo hilo. Mwenyekiti aliwaelekeza Watendaji wa TANESCO na REA kumpelekea Mama huyo umeme. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani humo Septemba 6, 2021.
Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Amos Maganga na Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale wakijadiliana jambo wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani Mwanza, Septemba 6, 2021.
Miundombinu ya Umeme katika Mtaa wa Shigunga, Eneo la Mandu Makaburini, wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza. Taswira hii ilichukuliwa Septemba 6, 2021 wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (hawapo pichani) kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Shigunga, Eneo la Mandu Makaburini, wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza, Ezekiel Shiula (kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (katikati) na Ujumbe wake, wakati wa ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (hawapo pichani) kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo, Septemba 6, 2021.
Mtoto Salma Seleman anayeishi Kishiri wilayani Nyamagana, Mkoa wa Mwanza akimwelezea Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kulia) na Ujumbe wake, hali ya upatikanaji umeme katika eneo hilo. Bodi ilikuwa katika ziara kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme, Septemba 6, 2021.
Veronica Simba – Mwanza
Bodi ya Nishati Vijijini imekagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi pamoja na miradi mingine inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mkoani Mwanza.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Wakili Julius Kalolo, akiwa amefuatana na mmojawapo wa Wajumbe wa Bodi Oswald Urassa, Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Amos Maganga pamoja na Wataalam mbalimbali kutoka REA na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), walikagua miradi hiyo Septemba 6, 2021.
Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya ziara hiyo, Wakili Kalolo alisema asilimia kubwa ya miradi imefikia hatua nzuri isipokuwa mmoja unaotekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi ya Segemcom.
Akifafanua, alieleza kuwa kwa mujibu wa Mkataba, Mkandarasi huyo anapaswa kuwa amekamilisha kazi yote ifikapo Novemba mwaka huu lakini hadi sasa amefikia asilimia 27 tu ya utendaji.
“Kwa maana hiyo, kwa miezi miwili iliyobaki, hatuoni ni kwa namna gani anaweza kukamilisha Mradi wetu,” alieleza Mwenyekiti.
Kufuatia hali hiyo, Wakili Kalolo alibainisha kuwa Bodi imemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa REA, ifikapo Jumatatu, Septemba 13, 2021 kumwandikia Mkandarasi husika kumtaka akamilishe kazi ndani ya muda sambamba na kumtaka awasilishe Mpango Kazi utakaotoa uhakika wa kufikia malengo hayo.
Aidha, Bodi ilielekeza kuwa, kupitia Andiko husika, Mkandarasi apewe Notisi inayoeleza nia ya kukusudia kuvunja Mkataba, endapo kufikia Septemba 30, 2021 atakuwa hajafikia asilimia 75 ya utekelezaji wa Mradi.
Sambamba na maagizo hayo, Bodi imewaagiza Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuwasilisha Mpango Kazi unaobainisha kazi itakayofanyika kila wiki, kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambako miradi hiyo inatekelezwa. Wakili Kalolo alisema lengo ni kuwawezesha viongozi hao kusaidia kufuatilia utekelezaji wa miradi husika.
Katika hatua nyingine, Bodi imeziagiza Idara za Uhusiano katika Taasisi za TANESCO na REA kushirikiana na viongozi wa vijiji, kuhamasisha wananchi ili wajiandae kupokea miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa katika maeneo yao.
Akifafanua, alieleza kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa na kuhamasishwa kuandaa makazi yao kupokea umeme kwa kutandaza mfumo wa nyaya kwa wale wenye uwezo, na kwa wasio na uwezo wahamasishwe kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Maganga alitoa wito kwa Wakandarasi, Wasimamizi wa Miradi kutoka REA na TANESCO kushirikiana na Viongozi wa Vijiji katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
“Tusipowashirikisha vizuri ndiyo kunakuwa na malalamiko mengi kwa sababu wanakuwa hawauelewi Mradi vizuri,” alisisitiza.
Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya miradi ya REA kwa Bodi, Msimamizi wa Miradi hiyo, Kanda ya Ziwa, Ernest Makale alibainisha kuwa Mradi wa Ujazilizi katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, unatekelezwa katika vitongoji 84 kwa gharama ya shilingi za kitanzania bilioni 6.8.
No comments: