BAKWATA MWANZA YATAHADHARISHA UUZAJI HOLELA NYAMA YA NGURUWE





NA BALTAZAR MASHAKA,Mwanza

BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza,limeibua malalamiko ya uzaji holela wa nyama ya nguruwe unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara jijini Mwanza na kutahadharisha utasababisha madhara ya kiimani.

Pia baadhi ya wamiliki wa baa likidai wanafungulia muziki kwa sauti ya juu jambo linalowakera wananchi na watu wengine wenye imani tofauti na kuwaomba wasimamizi wa sheria kusimamia hilo kwa weledi.

Kauli hiyo ilitolewa na Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikhe Hasani Kabeke juzi, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kuhitimishwa kwa maadhimisho ya mwaka mpya wa kiislamu wa 1443.

Alisema biashara ya uuzaji wa nyama ya nguruwe kufanyika holela katikati ya masoko na mitaani ni kero kwa watu na wananchi wengine wa imani za dini tofauti, hivyo serikali ilitazame hilo kwa kuwa ni kiashiria cha uvunjifu wa wa amani.

“Kuruhusu hilo lifanyike holela kunaweza kusababisha madhara kiimani, lakini niwaombe wanaofanya biashara hiyo wachukue tahadhari ikiwemo serikali yenyewe, wasituletee mgogoro unaoweza kusababisha uvunjifu wa amani,ifahamike kuwa hatutaki na hatulengi kuingilia biashara za watu, ”alisema Sheikhe Kabeke.

Pia kiongozi huyo wa kiroho mbali na hilo na kuuza nyama ya nguruwe alieleza kuwa baadhi wa wamiliki wa baa na kuitaja moja iliyopo Nyamanoro inapiga muziki na kufungulia kwa sauti ya juu kiasi cha kusababisha kero na kukosekana kwa usikivu kwenye makazi ya watu wanaoishi jirani na baa hiyo lakini bado ziko nyingine katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mwanza zinafanya hivyo.

“Ni toe rai wanaosimamia sheria za mazingira,wasimamie hilo ili kuondoa kero hiyo kwa wananchi maana wapo wagonjwa, watoto, wazee,wajawazito na wengine, wanahitaji kuishi sehemu tulivu bila kusumbuliwa kisaikolojia,nafahamu wenye baa wanatafuta riziki lakini isitumike kama kigezo cha kuwakera wengine,”alisema Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza.

Hivi karibuni akiwa wilayani Magu, Waziri wa wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Muungano na Mazingira, Seleman Jafo,alisema Jiji la Mwanza linaongoza kwa kelele za muziki zinazosababishwa na kumbi pamoja na nyumba za starehe.

Kutokana na kero na malalamiko hayo ya wananchi, alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Baraza na Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dk. Samwel Gwamaka, kushughulikia na kudhibiti kero hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Namba 20 ya Mwaka 2004.

Aliagiza wataalamu wa mipango miji kwenye halmashauri zote nchini washirikiane na NEMC, wahakikishe wanazingatia sheria katika kupanga miji,wapi nyumba za starehe, makazi na za ibada zinajengwa.

Pia wamiliki wa nyumba hizo za burudani wahakikishe nyumba ama kumbi zao zinafungwa vifaa vya kupima na kudhibiti sauti (Freequance Control)ili kuepusha kero hiyo na kutobughudhi jamii.

Jafo alisistiza kuwa Jiji la Mwanza linaloongoza kwa kelele zinazosabaishwa na nyumba za burudani na kusababisha malalamiko kutoka kwa wananchi wa jiji hilo, ili kudhibiti kero hiyo wataalamu wa mipango miji kwenye halmashauri zote nchini wazingatie na watumie Sheria Namba 20 ya mwaka 2004 na maboresho yake katika upangaji wa miji ili kulinda mazingira.

“Suala la kelele limetukutanisha mawaziri 8 kujadili kutunza mazingira na kupinga upigaji wa kelele,watu wameathirika kwa kupoteza usikivu kutokana na nyumba za burudani kupiga kelele za muziki bila kujali afya za watu wengine wakiwemo watoto,wajawazito,wazee na wagonjwa,”alinukuliwa Jafo na akaongeza;“Jiji la Mwanza linaongoza upande wa kelele hizo hivyo naamuagiza Dk.Samwel kushughulikia maeneo hayo yenye kelele wanayolalamikia wananchi ili kudhibiti hali hiyo lakini pia wataalamu wa mipango miji wazingatie sheria ya mazingira katika uendelezaji na upangaji miji.”

Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (wa tatu kutoka kulia) akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uuzwaji holela wa nyama ya nguruwe jijini humu.Picha na Baltazar Mashaka

 

No comments: