WAZIRI UMMY AZINDUA MPANGO MKAKATI WA PILI WA MIAKA MITANO WA TARURA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Ummy Mwalimu amezindua Mpango Mkakati wa Pili wa Miaka Mitano wa Wakala wa Barabara Vijiji na Mjini(TARURA) na kaulimbiu isemayo 'TARURA tunakufungulia barabara,  kufika kusipofikika.

Utekelezaji wa Mpango huo unalenga kuzitunza barabara zilizo katika hali nzuri na zilizo katika hali ya wastani kubaki katika hali hiyo ikiwa ni pamoja na kupunguza barabara zenye hali mbaya ili ziwe katika hali ya wastani na hivyo kuzifanya barabara hizo kupitika kwa Mwaka mzima.

Akizindua Mpango huo leo Jijini Dodoma,Waziri Ummy amewasisitiza kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuenzi Imani aliyoionyesha Rais Samia Suluhu Hassan kwao na dhamira ya kutatua changamoto za barabara kwa kutenga kiasi Cha  Shilingi Bilioni 966.43 katika bajeti ya mwaka 2021/2022 kwenye mfuko wa Tarura .

“Hapa tumekutana ili tukiondoka tuondoke na uelewa mmoja,mkishindwa kutimiza malengo mtanyooshewa vidole na hamtaaminika,tunataka tuone tija katika utekelezaji wenu,kauli mbiu hii isibaki kwenye karatasi,muitekeleze kwa vitendo,mwaka huu mmoja ndio wa kuwapima tujue je tatizo lilikuwa pesa au nini,pesa hizi zilizotolewa zitawapima.

Ameongeza kuwa,”Matarajio ya serikali kwa Tarura ni makubwa sana,tunaomba msituangushe,nendeni mkaonyeshe kuwa nyinyi ni taasisi sahihi ya kufungua barabara,”aliongeza Ummy.

Pamoja na hilo Waziri Ummy ametoa maelekezo matano ikiwemo uwepo wa ushirikishaji wa wadau wakiwemo madiwani katika uandaaji na utekelezaji wa mpango.

“Kuanzia sasa ni lazima mshirikishe mabaraza ya madiwani katika kupitia na kukubaliana vipaumbele vya barabara,nimekuwa napokea malalamiko ya kutoshirikishwa madiwani tubadilike katika hili,lakini pia niwaombe madiwani wenzangu tuzingatie ushauri wa wataalam wa Tarura,isije kutokea mkagawanya fedha hii kwa kila kata matokeo yake kazi inayofanyika haitoonekana,”alisisitiza.

Awali akizungumza katika Uzinduzi huo,Mtendaji Mkuu wa Tarura Mhandisi Victor Seff amesema Mpango huo unaanza kutekelezwa Mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 na utaongeza mtandao wa barabara kwa kiwango Cha lami kutoka kilomita 2,404.90 hadi kilomita 3,855.65.

Aidha kupitia Mpango huo zitaongezwa kilomita  29,116.57 za changarawe hadi kufikia kilomita 102,358.14,madaraja kutoka 2,812 hadi 6,620 ambapo kiasi Cha Shilingi Trilioni 3.6 kinakadiriwa kutumika.


No comments: