TABIBU WA TIBA ASILI DK. MPAPAI ANENA KUHUSU UVIKO 19

NA DENIS MLOWE, KYELA


MTABIBU maarufu wa Tiba asili na Tiba Mbadala Nyanda za Juu Kusini, Haji Hussein Mpapai almaarufu Dk. Mpapai amewataka wananchi kuzingatia miongozo inayotolewa na serikali kuhusu kuenea kwa maambukizi ya wimbi la tatu la Uviko 19.

Akizungumza na Jamvi la Habari, Dk. Mpapai wakati lilipomfata ofisini kwake kuhusu tiba za asili kama zina uwezekano wa kutibu ugonjwa wa Corona, Dk. Mpapi alisema kuwa katika tiba za asili kuna kila aina ya madawa lakini kwa sasa wananchi wafate miongozo inayotolewa na serikali katika kujikinga na kuachana na watu wanaopotosha kuhusu ugonjwa huo.

“Jamii ya watanzania ifike wakati wafahamu kwamba sisi matabibu wa tiba mbadala tunatibu sana wagonjwa mbalimbali lakini kwenye hili suala la Uviko 19 wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa na serikali na ni muhimu kwenda kupata chanjo ambao imekuwa ikitolewa “ alisema Dk. Mpapai.

Alisema kuwa kwa upande wake anauwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali ambayo dawa zake wamekuwa wakitumia watu na kupona ila kuhusu Uviko 19 lazima ufanyike utafiti wa kiasili kuweza kubaini ni mti gani unafaa kwa matibabu ya virusi hivyo na kuachana na matabibu wanaotumia ugonjwa huo kutaka umaarufu.

Alisema kuwa amekuwa akiwaimiza watu wengi kutumia barakoa, maji tiririka katika kunawa mikono na kuzingatia umbali wa mtu na mtu kwani ugonjwa wa corona ni janga la dunia na kuwataka watu wajitokeze kwa hiari kwenda kupata chanjo ambayo inatolewa bure katika vituo mbalimbali nchini.

Dk. Mpapai ambaye makazi yake ni Njombe, amejizoelea umaarufu katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nje ya nchi kwa kuwa mmoja wa Tabibu ambao dawa zake zimekuwa zikiwasaidia wengi na amekuwa wakijitolea mara kwa mara kusaidia jamii anazopita wakati wa matibabu yake ikiwemo kuchangia ujenzi wa madarasa, vituo vya afya ili kuweza kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Jamvi la Habari kuhusu matibabu ya tiba za asili na kienyeji walisema kuwa baadhi ya matabibu wamekuwa wakiwadanganya wananchi hivyo kitendo cha Dk. Mpapai kuunga mkono tiba za kisayansi ni kuonyesha kiasi gani anaijua kazi yake ya utabibu kwa njia ya asili.

Mmoja wa wananchi hao Lamso Malongo alisema kuwa baadhi yao waongo na kuwadanganya wananchi kwamba wanatibu corona kitu ambacho si kweli ila wananchi wanatakiwa kutumia njia sahihi katika kutafuta tiba na kupata chanjo za uviko 19.

Alisema kuwa Dk. Mpapai amekuwa mkweli kwa kuwataka wananchi kufata miongozo ya serikali katika kupambana dhidi ya gonjwa la corona ambalo ni tishio kwa sasa duniani na kukiri kwake lazima wafanye utafiti wa matibabu ya asili imeonyesha weledi katika matibabu anayotoa.

Naye Fransis Mwambasa alisema kuwa kuna uwezakano mkubwa wa tiba za asili kufanya kazi katika mapambano dhidi ya Corona lakini wakati kama huu ni muhimu watu kupata chanjo inayotolewa na serikali na kuzingatia miongozo inayotolewa nchini dhidi ya uviko 19.


 

No comments: