Rais Samia akutana na kuzungumza na Balozi wa Oman Nchini anaemaliza muda wake
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 12 Agosti, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman hapa nchini Mhe. Balozi Ali Bin Abdallah Bin Salim Al Mahrouqi aliyemaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Al Mahrouqi amempongeza Mhe. Rais Samia kwa utawala wake na kuishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa alioupata wakati alipokuwa akitekeleza majukumu yake.
Aidha, Mhe. Balozi Al Mahrouqi amesema Tanzania na Oman zina uhusiano mzuri na wa muda mrefu hivyo kuomba kuendelezwa kwa ajili ya maslahi ya nchi zote mbili pamoja na kuimarishwa biashara.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amemhakikishia Balozi Al Mahrouqi kuwa Tanzania itaendeleza na kudumisha ushirikiano wake na Oman kwa masalahi ya nchi zote mbili.
Mhe. Rais Samia amemjulisha Balozi huyo kuwa kwa sasa Tanzania inapitia sheria na sera zake mbalimbali za biashara ili kujenga mazingira mazuri zaidi ya biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika viwanja vya Ndege na Bandari ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya nchi hizi mbili.
Pia, Mhe. Rais amezitaka Tume za pamoja kati ya Tanzania na Oman kukutana na kuzungumza ili kuimarisha mambo mbalimbali baina ya nchi hizo.
Mhe. Rais Samia amemshukuru na kumpongeza Mhe. Balozi Al Mahrouqi kwa kazi nzuri ya uwakilishi wake hapa nchini katika kipindi cha miaka 4 kwa kudumisha uhusiano kati ya Oman na Tanzania.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Balozi wa Oman aliyemaliza muda wake hapa nchini Mhe. Ali Bin Abdallah Bin Salim Al Mahrouqi mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuaga leo tarehe 12 Agosti, 2021. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiagana na Balozi wa Oman aliyemaliza muda wake hapa nchini Mhe. Ali Bin Abdallah Bin Salim Al Mahrouqi mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma kwa ajili ya kuaga leo tarehe 12 Agosti, 2021. PICHA NA IKULU.
No comments: