KIONGOZI MBIO ZA MWENGE KITAIFA AWASIHI WANANCHI KULINDA MIUNDO MBINU YA MAJI

Na Zainab Nyamka,Michuzi TV

Jamii imetakiwa kuacha kuhujumu miundo mbinu ya maji bali wanatakiwa kuhifadhi na kulinda ili waendelee kupata huduma ya maji safi na salama na iwafae kwa vizazi vijavyo.

Hayo yamesemwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambashi wakati wa kutembelea na kukagua mradi wa maji wa Kibamba-Kisarawe uliotekelezwa kwa asilimia 100 na wananchi wanapata huduma.

Luteni Mwambashi amesema wananchi wanatakiwa kuendelea kulinda vyanzo vya maji na kuacha kuhujumu miundo mbinu kwani ni kosa kisheria.

Amesema, amekagua mradi huo wa kimkakati na bado unaendelea kutekelezwa kwa kasi ili wananchi
wa Kisarawe na maeneo mengine waendelee kupata huduma hiyo kwa uhakika zaidi.

“Nimeridhishwa na mradi huu na nawasihi DAWASA kuendelea kuhudumia wananchi wa Kisarawe , kazi mliyoifanya ni kubwa kuweza kufikisha maji Kisarawe,” amesema Luteni Mwambashi

Kwa upande wa DAWASA, akitoa maelezo ya mradi huo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu, Meneja wa DAWASA Kisarawe Alex Ng’wandu amesema mradi wa maji Kibamba-Kisarawe umetekelezwa kwa fedha za ndani na chimbuko la mradi huo ni  agizo la Hayati Dkt John Pombe Magufuli mwaka 2017 wakati wa uzinduzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu.

“Maji yanayokuja hapa yanatoka katika mtambo wa Ruvu Juu na mradi uliasisiwa na Hayati Dkt John Pombe Magufuli wakati akizindua mtambo huo Juni 2017, na Wizara ya Maji kupitia DAWASA ilitii maagizo hayo na kuanza utekelezaji Juni 2018 na kukamilika Desemba 2019,”amesema

Ng’wandu ameongezea  kuwa kwa sasa wakazi wa Kisarawe wanapata huduma ya maji na kazi ya kuunganisha huduma ya maji inaendelea kupitia Mkoa kazi wa DAWASA Kisarawe na jumla ya maunganisho 2030 yamefanyika.

Amesema mradi huu umejengwa na mkandarasi M/S Chico ya China kwa gharama ya Sh Bilion 10.6 ikujumuisha gharama za vifaa na ujenzi wa Tanki la maji la Lita Milion 6 na ulazaji wa mabomba kutokea Kibamba hadi Kisarawe kwa urefu wa Km 15.6

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kisarawe Dkt Yona Kabata amewashukuru serikali kupitia DAWASA kwa kuondoa changamoto ya maji katika mji wa Kisarawe kwa sababu imeenda kupunguza gharama za matumizi ya fedha  ambapo walikua wanatumia zaidi ya Milion 2 kwa mwezi na sasa ni ni kiasi cha Milion 1 kwa mwezi kinatumika.

Dkt Kabata amesema kuna baadhi ya vipimo vilikua vinashindikana kupimwa kwa masaa 24 kutokana na uhaba wa maji, mazingira ya vyoo kuwa vichafu na hata wodini ilifikia muda wagonjwa wanaletewa maji kutoka majumbani.

Katika hilo, Maeneo yaliyonufaika na mradi huo ni Kata ya Kisarawe na Kazimzumbwi huku maeneo mengine yatakayonufaika ni Kiluvya, Kwembe, Kisopwa, Mloganzila na maeneo maalumu ya Viwanda Kisarawe.

Aidha, ujenzi wa tanki hilo limeweza kupatikana kwa mradi mwingine wa maji wa Kisarawe-Pugu-Gongo la mboto utakaohudumia hadi maeneo ya Chanika, Majohe,  Vingunguti na Tabata Kinyerezi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambasha akipata maelezo ya mradi wa Kibamba- Kisarawe kutoka Mkurugenzi wa Uwekezaji na Miradi DAWASA Mhandisi Ramadhani Mtindasi  wakati wa kutembelea mradi huo uliotekelezwa kwa asilimia 100 na wananchi wanaendelea kufanyiwa maunganisho mapya.


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kisarawe Dkt Yona Kabata akiwashukuru Dawasa kwa kuwasaidia kuondoa changamoto ya maji katika Hospitali yao ambapo kwa sasa maji yanapatikana muda wote na mazingira yamekuwa safi.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2021 Luteni Josephine Mwambasha akizindua rasmi mradi wa Kibamba- Kisarawe uliotekelezwa kwa asilimia 100 na wananchi wanaendelea kufanyiwa maunganisho. Luteni Mwambashi ameambatana na Mkuu wa Wilaya Kisarawe Nickson George na viongozi wengine wa kitaifa
Wakazi wa Kisarawe wakinawa mikono baada ya kuingia ndani ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ili kujikinga na Maambukizi ya Uviko 19. Wakina mama hao wameishukuru serikali na DAWASA kwa kuwaletea mradi wa maji ulioondoa changamoto ya maji katika Hospitali hiyo

 

No comments: