CHUO CHA UFUNDI ARUSHA MBIONI KUKAMILISHA UTENGENEZAJI WA HELKOPTA NA GARI LINALOTUMIA UMEME
Charles James, Michuzi TV
MABORESHO makubwa yaliyofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) yamewezesha Chuo hicho kutengeneza Helkopta ambayo kufikia mwakani itakua kwenye hatua za majaribio.
Hayo yameelezwa na Mkufunzi wa Chuo hicho Idara ya Magari, Mhandisi Abdi Mjema wakati akizungumza na wandishi wa habari waliofika chuoni hapo katika ziara ya kuangalia maboresho yaliyofanywa na Wizara ya Elimu katika chuo hicho.
Mhandisi Mjema amesema ujenzi wa Helkopta hiyo ulianza mapema tokea mwaka 2015 ambapo lengo lao ni kuwa na chombo hicho kwa ajili ya kutumika kwenye uokozi wa majanga mbalimbali yanayotolewa ikiwemo ajali za moto.
" Lengo letu ni kuona tunatengeneza Helkopta yenyewe hapa tupo kwenye hatua za awali lakini tunaamini hadi kufikia mwakani tutakua kwenye hatua za majaribio ya chombo hiki na tunaamini tutaweza kukamilisha kama ambavyo tumepanga," Amesema Mhandisi Mjema.
Amesema asilimia 70 ya vifaa vilivyotumika kutengenezea Helkopta hiyo mpaka sasa wameagiza kutoka nje ya Nchi na kwamba kwa sasa wanategemea kuanza kutenegeneza vifaa wenyewe.
Aidha Chuo hicho pia kwa sasa kipo mbioni kutengeneza Gari litakalotumia umeme lakini pia wakiwa tayari wameshatengeneza baiskeli maalum zinazotumiwa na watu wenye ulemavu ambayo itakua inatumia umeme wa jua.
"Maboresho haya yaliyofanywa na Wizara ya Elimu kwenye Chuo chetu kwa kiwango kikubwa ndio yaliyochangia kuweza kukamilisha ubunifu huo wa Baiskeli ya kumsaidia Mlemavu lakini pia mpango wao wa kukamilisha Helkopta na gari hilo litakalokua linatumia umeme.
"Tumetengeneza Baiskeli kwa ajili ya Ndugu zetu wenye ulemavu ambayo itakua inatumia umeme wa jua, gharama yake ni Sh Milioni 2.5, tunashukuru wateja wamezipanda na kwa sasa tunapata oda nyingi za watu wenye kuzihitaji," Amesema Mhandisi David Raymond ambaye nae ni mkufunzi wa chuo hiko.
Aidha amesema Chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya umeme wa magari na magari yenyewe huku akitoa wito kwa watanzania kupeleka magari yao kwenye Chuo hicho pindi wanapohitaji matengenezo.
"Serikali yetu imefanya maboresho makubwa hadi kwenye Karakana zetu, tuna vifaa vya kuweza kutengeneza gari la aina yeyote, wananchi walete magari yao hapa yatengenezwe na watu wenye taaluma na waliobobea waache kupeleka kwa mafundi wa mtaani ili kuepuka madhara mbalimbali yanayojitokeza ikiwemo magari kulipuka,
Tunaishukuru Serikali kwa maboresho haya yametusaidia kupata vifaa vya kisasa ambavyo vimetusaidia sana katika ufundishaji, mfano hizi Injini mnazoziona ni sehemu ya vifaa ambavyo tumeletewa," Amesema Mhandisi Raymond.
Ametoa wito kwa mafundi ambao hawana taaluma hiyo kufika chuoni hapo kupatiwa mafunzo ya kitaalamu kwani ATC inatoa pia mafunzo ya kozi za muda mfupi.
Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha ATC, Mhandisi David Raymond akionesha mitambo ya kujifunzia ufundi magari kwa wanafunzi wa Chuo hicho. Mitambo hiyo ni sehemu ya maboresho ambayo yamefanywa na Serikali.
Mkufunzi wa Chuo cha Ufundi Arusha, Mhandisi David Raymond akionesha Baiskeli maalum iliyotengenezwa chuoni hapo mahususi kwa ajili ya Watu wenye ulemavu. Baiskeli hiyo inatumia umeme wa jua.
No comments: