Agizo la waziri mkuu latekelezwa Manyara, wafanyabiashara wamiminika
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgud_ELbptVL7gy2Z1S-8wN2w-paDKyU1m53zDXi1aZr-K6So6c17ddCDM9LZTH2J5ioAby3i9RAY5IFhfxWIDGJUHf4FoqxqCcA7OOMQ1Udt0G8InQl4xhQ5koqe-cIwMXcf09Hgu_KAHt/s16000/MAKONGORO+SIMANJIRO.jpg)
Na John Walter-Manyara
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere, amesema agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la shughuli zote za ununuzi na uongezaji thamani wa madini ya Tanzanite, kufanyika Mirerani baada ya siku 90 linaendelea kutekelezwa baada ya wafanyabiashara 46 kufungua ofisi Mirerani.
Makongoro akizungumza akiwa wilayani Simanjiro, amesema Mkoa umefanikisha mambo manne ili kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa Mirerani juu ya shughuli za Tanzanite kufanyika Mirerani.
Amesema majengo mawili yameshatengwa kwa ajili ya uuzaji wa madini hayo na yameshaanza kutumiwa na wafanyabiashara 49 wa madini hayo.
Amesema hatua zinazoendele ni upimaji wa eneo la kanda maalum ya kiuchumi (Manyara Special Economic Zone) ili kuwagawia wafanyabiashara wa madini waweke miundombinu yao na maeneo ya makazi.
"Serikali kwa upande wake inaendelea kuingiza miundombinu muhimu ya kuwezesha huduma za maji, umeme, barabara na nyingine kama itakavyohitajika," amesema Makongoro.
Amesema pia kupitia eneo hilo lililotengwa limepangwa kuwa na huduma muhimu za kijamii zikiwemo hoteli, migahawa, kituo cha polisi na maegesho ya magari.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa Julai 7, 2021 wakati akizindua kituo cha Tanzanite Magufuli aliagiza hadi kufika Agosti 10, 2021 kuhakikisha utaratibu wa kununua madini ya Tanzanite kupitia soko la madini Mirerani unaanza kufanyika ufanyike katika mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara.
No comments: