TET, DIT WASAINI MKATABA KUANDAA MITAALA YA SHULE ZA UFUNDI NCHINI
Na Humphrey Shao, Michuzi Tv.
TAASISI ya Elimu Tanzania(TET) imetiliana saini mkataba na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) Kwa ajili ya uandaaji wa mitaala ya shule za ufundi nchini.
Mkataba huo umesainiwa leo Juni 17,2021 mkoani Dar es Salaam katika Viwanja vya TET na Kushuhudiwa na katibu mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Donald Akwilapo.
Akizungumza kabla ya utiaji huo wa saini, Dk.Akwilapo amesema kumekuwepo na kikubwa cha cha muda mrefu kutoka kwa wadau kuhusu uboreshaji wa mitaala katika shule za ufundi nchini, hivyo Serikali ya Awamu ya sita imesikia kilio hicho ndio maana leo wako hapa.
"Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania ,Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kutekeleza kilio cha wadau kwa kuandaa mitaala mipya ya ufundi inayoendana na wakati " amesema Dk. Akwilapo
Ametoa mwito kwa wataalamu wote ambao watahusika katika kuandaa mitaala hiyo waweze kuambatanisha na andiko la vifaa vya kisasa vinavyoendana na wakati katika karakana zitakazojengwa shuleni hapo.
Amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika mpango wa uboreshaji wa mitaala hiyo hivyo inatakiwa iwe na karakana za kisasa kama ilivyo katika shule ya Arusha Tec.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TET, Aneth Komba Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiamini taasisi hiyo kwa kuirejeshea majukumu ya uandaaji mitaala,jambo ambalo miaka ya nyuma lilisitishwa.
Amesema kwamba wao taasisi wamejipanga vema lakini wanomba washirika wao DIT kuendelea kushirikiana nao na kuwa bega kwa bega katika usimamiaji wa shughuli hiyo muhimu kwa Taifa.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba na Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba wakisaini makubaliano ya uandishi wa vitabu 32 vya kiada vya masomo ya ufundi shule za Sekondari nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dr Donald Akwilapo akizungumza na wadau wa elimu waliofika katika hafla ya utilianaji saini . Mkurugenzi wa Tasisi ya Elimu Tanzania TET ,Aneth Komba akizungumza na wadau wa elimu.
No comments: