SERIKALI YAANZA KUWASAKA WEZI WA MAFUTA DAR
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam imesema kuanzia kesho inaanza zoezi la kuwasaka wezi wa mafuta katika eneo la Kigamboni ikiwa ni baada ya kubainika upotevu wa mafuta hayo katika eneo hilo na kusababisha hasara kubwa.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Amos Makalla katika kikao kazi na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama sambamba na wadau wa mafuta baada ya kusikiliza kero zao.
Makalla amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa itapita sehemu hizo ili kubaini upotevu huo na kuchukua hatua ikiwa pamoja na kukagua miundombinu ya bomba husika la mafuta, pia ameagizwa Mkurugenzi wa bandari kuangalia kwa kina kupitia vifaa maalum vinavyobaini wizi huo.
Aidha, Makalla amesema wote waliojiunganishia bomba hilo wajisalimishe kabla ya Kamati ya Ulinzi haijapita maeneo hayo yaliobainika kupita Bomba hilo, amesema hatua kali zitachukuliwa kwa wote waliobanika kujiunganishia Bomba hilo.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Wadau wenyewe wa mafuta tunaanza zoezi la kupita eneo kwa eneo, mtaa kwa mtaa katika eneo lile la Kigamboni kubaini wale wote waliojiunganishia Bomba na kusababisha hasara kubwa kwa Serikali yetu”, amesema Makalla.
Pia Makalla ametoa wito kwa wadau hao wa mafuta kufunga ‘Flow Meters’ ili kujihakikishia upotevu wa mafuta hayo unakoma, amemuagiza Mkurugenzi wa Bandari kufuatilia kero hivyo baada ya utaratibu kukamilika.
No comments: