WAPO WAJASIRIAMALI WENGI LAKINI HAWANA MAWAZO YA KIBIASHARA,WENGI WAO WANARIDHIKA NA KILE WANACHOKIUZA-PROF MJEMA
Na Jusline Marco-Arusha
Mwenyekiti wa wakuu wa taasisi zilizomo ndani ya wizara ya viwanda na biashara ambaye pia Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Prof.Emmanuel Mjema amesema ili kuweza kukabiliana na changamoto ya bidhaa kutokuwa na masoko,taasisi husika zinapaswa kuweka mipango biashara itakayo wawezesha kuboresha bidhaa zao na kupata masoko ya uhakika.
Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea taasisi hizo Prof.Emmanuel amesema lengo ni kutambua fursa za mashirikiano baina ya taasisi hizo ili kuweka lebo za viwango ambazo zitawezesha bidhaa hizo kuuzika ndani na nje ya nchi.
Aidha amesema kuwa katika taasisi walizotembelea ikiwemo Taasisi ya TEMDO na CAMATEC wamekuta bidhaa nyingi lakini hazifahamiki nje ya taasisi zao ambapo ameona ni maeneo muhimu ya kuwasaidia katika biashara,kuweka fursa za kibiashara zaidi kwa kuhakikisha wanatengeza mipango biashara utakao wezesha bidhaa zao kuuzika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
"Wapo wajasiriamali wengi lakini hawana mawazo ya kibiashara kutokana na wengi wao kuridhika na kile wanachokiuza, hivyo niwatake wajasiriamali waweze kufikiria fursa za masoko nje ya Tanzania na hiyo itawezekana kama tutaboresha ubora wa bidhaa tunazotengeneza."Alieleza Prof.Mjema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo Tanzania,Silivester Mpanduji amesema kama Shirika la kuhudumia viwanda vidogo wanatoa mikopo kwa wajasiriamali kuanzia shilingi Milioni 5 ambapo kwa kushirikiana na Benki ya CRDB wanatoa mpoko wa shilingi Milioni 10 hadi Milioni 50.
"Lakini hivi karibuni tumeanzisha mahusiano na wenzetu wa Azania Benki,NSSF pamoja na VETA ambapo kwa kuanzia sasa mtanzania anaweza kupata mkopo kati ya shilingi milioni 8 hadi milioni 50 na wajasiriamali wanaokuwa,wanaweza kupata mkopo kati ya shilingi milioni 50 hadi milioni 500 na kwa kufanya hivyo watanzania wengi wataweza kuanzisha na kukuza viwanda vyao."Alisema Mpanjuli
Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Arusha Bi.Nina Nchimbi amesema uwezo wa viongozi hao kufanya ziara hiyo umewasaidia kuweza kuona fursa mbalimbali na kuweza kufanya nao kazi kwa karibu na kushirikiana ili kufikia Tanzania ya viwanda ya mafanikio.
"Changamoto kuu ambayo tunayo ni upatikanaji wa taarifa sahihi kwetu sisi kama taasisi lakini upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wajasiriamali kuweza kutambua na kuona taasisi zilizo chini ya viwanda na biashara zinafanya nini au zinahusika na nini."Alisema Bi.Nina
Sambamba na hayo amesema kuwa mikakati yao ni kuweza kushirikiana na taasisi hizo ili kuweza kufikia mafanikio wanayoyahitaji kwa ajili ya wajasiriamali wao.
Mwenyekiti wa wakuu wa taasisi zilizomo ndani ya wizara ya viwanda na biashara ambaye pia Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara, Prof.Emmanuel Mjema
No comments: