Tulila kivutio kipya cha utalii mkoani Ruvuma
Hata hivyo maporomoko ya Tulila ndipo kuna mradi wa umeme wa maji toka maporomoko ya mto Ruvuma,unaomilikiwa na watawa wa Benedictine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo kuu la songea.
Mradi huu unazalisha megawati tano ambazo zilimaliza tatizo la umeme katika mji wa Songea kabla ya Mkoa wa Ruvuma kuingizwa katika grid ya Taifa.
Kutoka Songea mjini hadi Tulila ni takribani kilometa 89.Kivutio hiki bado hakifahamiki na wengi hivyo kinatakiwa kutangazwa ili kifahamike ndani na nje ya nchi.
Tulila ni eneo lenye mandhari nzuri ya kuvutia unaweza kufanya utalii wa kupiga picha, kuogelea, kuendesha mtumbwi pia kuna fukwe nzuri kutoka katika mto Ruvuma.
Uchunguzi umebaini kuwa bwawa la kuzalishaji umeme lenyewe pekee ni kivutio tosha cha utalii wa majini na katika eneo hili kuna aina adimu za ndege ambao ni kivutio cha utalii wa kuona ndege.
Utalii ambao unaweza kushamiri hivi sasa katika Mkoa wa Ruvuma na Taifa kwa ujumla ni utalii wa ndani ambapo katika eneo la Tulila watawa wanamiliki eneo lenye ukubwa wa hekari 1000.
Watawa katika eneo la bwawa wamewekeza kwenye ufugaji wa samaki wa aina mbalimbali na kupanda miti aina ya mitiki yenye thamani kubwa kwa sababu hekari moja ya mitiki inaweza kumuingizia mkulima hadi shilingi milioni 400.
Afisa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema uchunguzi umebaini kuwa samaki hao wanavutia makundi ya ndege wakiwemo tai ambao wanakula samaki.
Watawa hao wanafuga mbuni ,bata mzinga na aina nyingine za ndege ambao ni kivutio cha utalii ambapo Tulila itakuwa maalum kwa ajili ya utalii wa kuona ndege wa aina mbalimbali.
Maporomoko ya Tulila yapo kilometa sita toka Pori la Akiba la Liparamba lenye wanyama wa aina mbalimbali hivyo watalii watakaotembelea Liparamba wanaweza kufika kwenye maporomoko ya Tulila ambako wanaweza kupata malazi na chakula kwenye hoteli za kisasa za kitalii zinazomilikiwa na watawa hao.
Inaelezwa tembo wa Liparamba pia wanafika kwenye maporomoko ya Tulila na kwamba majira ya asubuhi na jioni makundi makubwa ya ndege na viboko wanafika katika eneo hilo kunywa maji na kula chakula.
Mto Ruvuma ambao Chanzo chake ni milima ya Matogoro iliyopo nje kidogo ya mji wa Songea,ni miongoni mwa mito maarufu barani Afrika unamwaga maji yake Bahari ya Hindi.
No comments: