RIPOTI YA KAMATI MAALUMU KUHUSU MWENENDO WA TATHIMINI YA CORONA YAWASILISHWA KWA RAIS SAMIA IKIWA NA MAPENDEKEZO 19, LIMO LA CHANJO HURU
Na Mwandishi Wetu ,Michuzi Blog
KAMATI ya kitaaluma iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutafiti juu ya mwenendo wa ugonjwa wa Corona (Covid-19) imewasilisha rasmi ripoti yake kwa Rais huku ikitoa mapendekezo 20 ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kwamba kamati ilifanyia kazi hadidu za rejea 12 zilizohusu maeneo mbalimbali ya tathmini ya mwenendo wa ugonjwa pamoja na afua za udhibiti wa COVID-19 ikiwemo chanjo hapa nchini, kikanda na kimataifa.
Akizungumza leo Mei 17,2021,Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Said Aboud mesema tangu kuingia kwa ugonjwa wa COVID-19 nchini Machi 2020, Tanzania imekumbwa na mawimbi mawili makubwa na hivi sasa kutokana na mwenendo wa ugonjwa huo katika mataifa mengine duniani na kuna tishio la kutokea kwa wimbi la tatu hapa nchini.
Kuhusu mapendekezo ya kamati hiyo baada ya kufanya tathimini ya ugonjwa huo inapendekezwa Serikali ihuishe mipango ya dharura (Contigency and Response Plans) katika ngazi zote kwa ajili ya kukabiliana na majanga likiwemo janga la ugonjwa wa COVID-19, Serikali itoe taarifa juu ya uwepo wa ugonjwa wa COVID-19 na ichukue hatua madhubuti kuimarisha hatua zote za afua za kinga (interventions) katika ngazi zote ili kuepusha wimbi la tatu la ugonjwa huo.
Profesa Aboud amesema pendekezo lingine niWataalamu wa afya watimize wajibu wao kitaalamu, kwa kuzingatia weledi, miiko na maadili katika kuelimisha, kukinga na kutibu ugonjwa wa COVID-19 nchini. Tanzania ishiriki ipasavyo katika maamuzi na itekeleze maazimio ya kikanda na kimataifa iliyoridhia katika jumuiya za EAC, SADC, AU na WHO.
Kuhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19: Kamati inashauri Serikali kwa kutumia vyombo vyake iendelee na hatua kuelekea kuruhusu matumizi huru ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa COVID-19 kwa kutumia chanjo zilizoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani ili kuwapa fursa ya kinga wananchi wake kwa kuwa kupitia uchambuzi wa Kamati, chanjo hizo zina ufanisi na usalama unaokubalika kisayansi.
Pamoja na mapendekezo haya, Kamati Huru ya Kitaifa ya Ushauri wa Chanjo (NITAG) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ziendelee kushirikishwa katika kutoa ushauri na kudhibiti chanjo hizo; Kipaumbele cha utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 nchini kwa kuanzia kiwe katika makundi yafuatayo kwa umuhimu:
Wahudumu katika vituo vya kutolea huduma za afya na watumishi walio katika mstari wa mbele wa utoaji wa huduma (frontline workers) mathalani watumishi sekta ya utalii, hoteli, mipakani, viongozi wa dini na mahujaji; Wazee na watu wazima kuanzia umri wa miaka zaidi ya 50, Watu wazima wenye maradhi sugu mengine (comorbidities) mathalani kisukari, shinikizo la damu, maradhi ya mfumo wa upumuaji, magonjwa ya figo.
Pia wengine ambao wanatakiwa kupewa kipaumbele ni Watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.Kamati imependekeza kufanya uhamasishaji na maandalizi ya upokeaji, utunzaji, usafirishaji na utoaji wa chanjo na wananchi wawe huru kuamua kuchanja au la. Serikali iratibu upatikanaji wa chanjo kwa watumishi wa taasisi za kimataifa walioko nchini.
"Kamati imependekeza Serikali ya Tanzania ijiunge na COVAX Facility kwa kuwasilisha andiko la kupatiwa chanjo, kwa kutumia fursa inayotolewa na GAVI, Serikali itumie fursa zilizopo wakati huu wa janga la COVID-19 kuanza mchakato wa uanzishaji wa viwanda vya kutengeneza chanjo, Serikali iimarishe huduma za uchunguzi kwa kuijengea uwezo Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na maabara nyingine nchini ili kupanua wigo wa upimaji wa ugonjwa wa COVID-19,"amesema Profesa Aboud.
Pia Serikali ijenge uwezo wa ndani wa utambuzi wa virusi anuai vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza, Serikali itoe takwimu sahihi za ugonjwa wa COVID-19 kwa umma na Shirika la Afya Duniani ili wananchi wapate taarifa sahihi toka Mamlaka za Serikali na kuheshimu makubaliano na kanuni ambazo nchi iliridhia.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikamilishe mwongozo mpya wa matibabu ya ugonjwa wa COVID-19, Serikali iendelee kuhakikisha kuwa matumizi ya tiba asili na tiba mbadala katika mfumo rasmi wa tiba za kisasa yanazingatia misingi ya kisayansi,
Serikali iendelee kutoa fursa na kuwawezesha wanasayansi kufanya tafiti kwa kufuata miiko, maadili na taratibu zilizowekwa ili kuimarisha kinga, tiba, uchunguzi wa ugonjwa wa COVID-19 na athari zake katika jamii nchini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo Profesa Aboud amesema kamati hiyo inapendekeza pia Serikali iendelee kuzingatia mazingira ya kitanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa COVID-19 katika kuamua kuweka au kutokuweka shuruti ya kujifungia (lockdown) na kuwa na ubunifu ili kuruhusu ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta zinazochangia katika uchumi, Wizara yenye dhamana ya fedha na uchumi ifanye tathmini ya kina ya athari za janga la COVID-19 na kuweka mpango madhubuti wa haraka wa sasa, wa muda wa kati na wa muda mrefu unaotekelezeka ili kukuza uchumi wa nchi.
Mengine ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ziendelee kushirikiana ipasavyo katika hatua zote za kukabiliana na janga la COVID-19 pamoja na majanga mengineyo ikiwemo utoaji wa nyaraka za kimataifa kama vile Travel Advisory Note, Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kutekeleza ipasavyo jukumu la uratibu na kutoa rasilimali husika wakati wa majanga ya kitaifa na kimataifa kama ugonjwa wa COVID-19 kwa kushirikisha ngazi na sekta zote.
Pia amesema Serikali ikamilishe malipo ya madeni ya watoa huduma na watumishi waliokuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 ili kuongeza ari na tija ya udhibiti wa ugonjwa huo. Serikali iendelee kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na vyombo vya habari katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa COVID-19.
No comments: