MKOA WA RUKWA WAJIVUNIA MAFANIKO KATIKA TASNIA YA UTOAJI WA HAKI
Na Mwandishi Maalum
Mkoa wa Rukwa umeeleza mafanikio chanya katika Utoaji Haki, mafaniko ambayo yamewafanya wananchi wa mkoa huo kuishi kwa amani na usalama na hivyo kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamo katika taarifa fupi ya Mkoa huo kuhusu hali ya utekelezaji wa Hakijinai taarifa ambao imeainisha mafanikio na changamoto.
Taarifa hiyo ilisomwa na Wakili Frida Hava wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, Dkt. Laurean Ndumbalo Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Dkt. John Jingu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wadau wa Hakijinai Mkoa wa Rukwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mafanikio hayo yamechangiwa pamoja na mambo mengine na uwepo wa , na ushirikiano wa Idara ,Ofisi na Taasisi mbalimbali zinazoisaidia Mahakama katika kutenda haki.
Baadhi ya Ofisi hizo ni kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Huduma kwa Jamii na Sheria ya Majaribio na Ujenzi wa Tabia.
“Uwepo wa vyombo hivyo na vingine katika mkoa wetu umeleta mafaniko chanya ambayo yametokana na utendaji kazi wake. Utoaji haki unawafanya Wananchi wa Mkoa wa Rukwa kuishi kwa amani na usalama hivyo kuweka mazingira rafiki kwa maendeleo ya Mkoa na nchi kwa ujumla” inasomeka taarifa hiyo.
Taarifa hiyo pia imeeleza kwamba, malalamiko mengi ya wananchi yamekuwa yakishughulikiwa na vyombo hivyo vya utoaji haki kwa weledi na ufanisi mkubwa na hivyo kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi ambayo yangefikishwa katika Ofisi za Serikali na kushughulikiwa pasipo kufuata misingi ya utoaji wa haki.
Aidha Mkoa wa Rukwa unajivunia kuendelea kupungua kwa msongamano wa wafungwa gerezani hasa baada ya kuanzishwaji wa Huduma kwa Jamii na Sheria ya Majaribio ya Ujenzi wa Tabia mwaka 2018 ambapo hadi sasa mkoa una wataalamu wawili wanaoshughulika na utoaji wa huduma hiyo.
“Kwa rejea, tangu mwezi Agosti, 2018 hadi Mei, 2021 Idara ya Huduma za Uangalizi imefanikiwa kutoa jumla ya wafungwa wa kifungo cha nje 136. Kwa kuwa Idara hii inahamasisha utoaji wa Adhabu Mbadala imesaidia kupunguza gharama kwa Serikali katika kuwahudumia wafungwa na kuwasaidia wahalifu wadogo wasiende kujifunza mbinu mpya za uhalifu pindi wanapokuwa gerezani”.Inasema taarifa.
Pamoja na mafakio hayo , Mkoa wa Rukwa na kwa mujibu wa taarifa hiyo, unakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa Hakijinai.
Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na, kwa baadhi ya vyombo vinavyohusika kutoa haki kulalamikiwa kujihusisha na rushwa na kusababisha haki ya wananchi kupotea kabisa au kuchelewa kabisa.
Changamoto nyingine ni kwa baadhi ya vyombo vya utoaji haki kuingiliwa na vyombo vingine visivyo na mamlaka ya kutoa haki mfano Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) huingiliwa utendaji wake na watendaji wa Serikali.
Changamoto nyingine ni kwa baadhi ya watuhumiwa kulalamikia kitendo cha kubambikiziwa kesi na walalamikaji kwa kushirikiana na Idara za kutoa haki ambazo hazina uaminifu kwa lengo la kuwakomoa au kulipa kisasi.
Kutofikishwa mahakamani kwa kesi nyingi za mahabusi kwa kigezo cha upelelezi kutokamilika kunawafanya mahabusu hao kukaa muda mrefu gerezani na kuisababisha Serikali hasara na kuchelewesha haki kwa mahabusu hao ni moja ya changamoto inayoukabili Mkoa huo katika uotaji ya Hakijinai
Changamoto nyingine ni wafungwa wengi kushindwa kukata rufaa kutokana na kukosa nakala za hukumu au nakala za hukumu kucheleweshwa sana kutolewa, hali hii imepelekea wafungwa wengine kumaliza kifungo bila kutekeleza haki yao ya kukata rufaa.
Mkoa huo wa Rukwa pia unakabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa wakalimani wakati wa kusikiliza kesi au malalamiko yao hasa wa lugha adimu za kigeni wakitolea mfano lugha ya kichina na lugha ya alama kwa watu wenye ulemavu.
Changamoto ya kukosekana kwa wakalimani wa lugha za kigeni na alama kumeelezwa kukwamisha chombo kinachohusika na mwenendo wa shauri fulani kushindwa kuendelea hadi hapo mkalimani atakapopatikana.
Mwamko hafifu wa Wananchi katika kutoa ushirikiano kwa wahanga wa matukio ya uhalifu hasa yanayohusu maadili kama mimba za utotoni, ubakaji, ulawiti, ndoa za utotoni na udhalilishaji.
Akijibu baadhi ya changamoto hizo, ikiwamo ya baadhi vyombo vya utoaji haki kuingiliwa na vyombo visivyo na mamlaka ya utoaji haki, Katibu Mkuu Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome ametaka jambo hili liachwe mara moja na kila chombo kitekeleze majukumu yake bila kuingilia chombo kingine.
Amewasisitiza watumishi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, maadili na miongozo ya utumishi wa umma na kamwe wasipindishe sheria.
Kuhusu baadhi ya watendaji katika vyombo vya utoaji wahaki kulalamikiwa kuchukua rushwa, Profesa Mchome ameitaka TAKUKURU kutimiza wajibu wake.
Imetolewa na Maura Mwingira
Mrakibu wa Magereza Mkoani Rukwa SP Daniel Ndamgilire akichangia majadiliano kuhusu hali ya utoaji haki ilivyo katika Mkoa wa Rukwa
Makatibu Wakuu, Katiba na Sheria, Utumishi na Maendeleo ya Jamii, JInsia, Wazee na Watoto wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi wa wadau wa vyombo vya Utoaji haki, mara tu baada ya kikao chao kilichofanyika siku ya Alhamisi ambao mafanikio na changamoto za utoaji haki katika mkoa huo zilijadiliwa. Makatibu Wakuu hao wapo katika ziara ya kikazi ya kawaida ya kutembelea Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi
No comments: