Dkt.Abbasi asisitiza Weledi kwa Wafanyakazi wa TSN


Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amewaasa Wafanyakazi  wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN)  kufanya kazi kwa weledi ili kupata mafanikio zaidi katika Kampuni hiyo na nchi. 

Dkt. Abbasi ameyasema hayo Mei 4, 2021 alipofanya ziara kwenye Kampuni hiyo  kukagua utendaji wa kazi na  kujadiliana  na Menejimenti na Wafanyakazi namna bora ya kuongeza ufanisi wa kazi.

Amesema TSN ni Kampuni ya Serikali inayoaminika  hivyo watumishi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi ili kuendelea kutoa taarifa zenye ubora zinazozingatia Misingi ya Taaluma ya Uandishi wa Habari.

Amewashukuru wafanyakazi hao kwa  kuendelea kutoa ushirikiano kabla na baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  kushika tena wadhifa huo hivi karibuni. 

“Asanteni kwa ushirikiano mliouonesha kwangu kipindi nina kofia ya Msemaji Mkuu wa Serikali hadi sasa nimeenda kuwa Katibu Mkuu, hamkuchoka na tulifanya kazi usiku na mchana, tuendelee kushirikiana bila kuchoka, ili kukidhi matarajio ya Rais wetu na wananchi kwa ujumla” amesisitiza Dkt. Abbasi.

Akiwa katika ziara hiyo, pia ameitaka  Menejimenti ya TSN kujali maslahi ya wafanyakazi  wote ili kuleta ufanisi wenye tija.

Naye Kaimu Mhariri Mtendaji wa Kampuni hiyo Bibi. Tuma Abdallah amempongeza  Katibu Mkuu huyo kwa kuaminiwa tena katika nafasi hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.

Hii ni ziara ya kwanza  ya kikazi aliyoifanya   Katibu Mkuu,  Dkt. Abbasi mara baada ya kuteuliwa tena hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo.

No comments: