MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE WATOA SH MILIONI KUSAIDIA WATOTO WENYE UHITAJI JIJINI DODOMA
Charles James, Michuzi TV
MFUKO wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) umetoa msaada wenye thamani ya fedha za kitanzania Sh Milion nne na laki tano kwa jili ya kuwapatia mahitaji muhimu watoto wanaolelewa katika Nyumba ya Matumaini Miyuji kilichopo jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa (UCSAF), Justina Mashiba amesema wameamua kutoa mchango huo kama Taasisi kwaajili ya kuchangia huduma mbalimbali zinazotolewa katika kituo hicho.
Amesema kupitia Mfuko huo wameona ni vyema kwa kipindi hiki cha siku ya wanawake duniani kuweza kujitoa kwa kuwaletea mahitaji hayo ikiwemo chakula, na mafuta.
“Sisi kama wazazi tunawajibu wa kuwahudumia watoto wetu pasipo kujali ni wakuwazaa wenyewe ama lah, hivyo tumeamua kukusanyika kama Mfuko wa Mawasiliano kwa pamoja hususani wiki hii ni siku ya wanawake duniani hivyo tuje kituoni hapa kuwapatia chochote watoto hawa” Amesema Mashiba.
Aidha Mashiba amewataka wana jamii wote kuwa na desturi ya kutembelea vituo mbalimbali kwa ajili ya kuwafariji watoto hao ikiwemo kuwasaidia kuwapatia mahitaji mbalimbali kadri wawezavyo.
Amesisitiza kuwa wanawake waache dhana mbaya za ukatili dhidi ya watoto kwa kuwafanyia matukio mbalimbali yasiyofaa badala yake wawe na kipaumbele kama wazazi katika kusimamia malezi bora yatakayomjenga mtoto katika maisha yake.
“Nitoe rai hususani kwa wazazi wa kike wanaotenda vitendo viovu kwa watoto kuacha mara moja kwani wao ni wazazi haijalishi ni wakuwazaa ama sio, bali wawatendee matendo mazuri” Amesema Mashiba.
Kwa upande wake Mlezi wa Kituo hicho cha Nyumba ya Matumaini, Sista Olea Kyala, ameishukuru Taasisi hiyo kwa moyo waliouonesha kwa kujitoa katika kuwasaidia watoto hao na kuwaomba waendelee na moyo huo wa kuwasaidia wahitaji wengine kwenye vituo mbalimbali hapa Nchini.
“Nawashuruku sana kwa hatua mliyo ifikia mmeamua kuja kushirikiana na sisi na kwa kweli Mungu awabariki kwa hiki mlicho kitoa kizidi kuwaletea neema zaidi kweli tumefurahi na tutazidi kuwashukuru” Amesema Sista huyo.
No comments: