MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ZANZIBAR AITEMBELEA FAMILIA YA MAREHEMU SHAWAL ZAM UNGUJA
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, leo hii aliitembelea familia ya Marehemu Maalim Shawal Zam iliyopo Mombasa kando kidogo ya kitovu cha Mji wa Unguja kwa ajili wa kuwahani kutokana na kuondokewa na Mzee wao huyo.
Maalim Shawwal aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita (Machi 5) katika Hospitali ya Al Rahma alikuwa rafiki mkubwa wa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
Makamu wa Kwanza wa Rais ameiambia familia hiyo kwamba baada ya mzee kufariki dunia, warithi wake wana wajibu wa kuyaendeleza yote mema aliyoyawacha mzee, ndio maana naye hatawacha kuwa karibu na watu ambao mtangulizi wake, Maalim Seif, alikuwa karibu nao.
Katika uhai wake, Maalim Shawwal aliwahi kuwa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Uweleni iliyopo Mkoani kisiwani Pemba, na baadaye akawa Mkaguzi wa Maskuli ya Zanzibar chini ya Wizara ya Elimu kabla ya kushikilia wadhifa wa Mkurugenzi Idara ya Elimu Msingi na Kati na hatimaye kuhamishiwa Ofisi ya Waziri Kiongozi alikohudumu kama Mkurugenzi wa Uratibu hadi alipostaafu rasmi.
Mheshimiwa Othman amesema Maalim Zam alikuwa miongoni mwa watu muhimu sana visiwani Zanzibar na hivyo kama familia na Wananchi wa kawaida hawana budi ila kuyafuata yale mema kutoka kwake.
“Tuendelee kumkumbuka Mzee Shawwal kwa dua kwani huko aliko ndilo jambo kubwa analohitaji kwa sasa kutoka kwetu,” amesema Makamu huyo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Maalim Shawwal ameacha Vizuka wawili, Watoto 11, Wajukuu 48 na Vitukuu 21.
SISI NI WA MUNGU NA KWAKE TUTAREJEA. Allah amrahamu na amlaze mahala pema peponi. Amin
No comments: